Marekani yaishtumu China kwa kufanya kampeni ya ujasusi
Marekani na washirika wake wa karibu wameishtumu China kwa kufanya kampeni ya ujasusi wa kimataifa, madai ambayo yamepingwa vikali na China.Marekani, jumuiya ya muungano wa NATO, Umoja wa Ulaya, Australia, Uingereza, Canada, Japan na New Zealand zimelaani ujasusi wa China, wakati Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akisema ujasusi wa China ni tishio kubwa kwa usalama wa kitaifa na kiuchumi.Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje katika ubalozi wa China nchini Marekani Liu Pengyu amepuuza madai hayo huku naye msemaji wa wizara ya mambo wa China Zhao Lijian akisema madai hayo yalitolewa kwa lengo la kisiasa. Wakati hayo yakiarifiwa, wizara ya sheria ya Marekani imewafungulia mashtaka ya udukuzi raia wanne wa China uliolenga kampuni kadhaa, vyuo vikuu na mashirika mengine ndani na nje ya Marekani.