Ni watu wenye ushawishi katika uongozi wa kila siku wa nchi zao, hata hivyo si kila siku utasikia juu ya maisha yao na vipawa vyao. Hawa ni wenza wa marais, ambao baadhi yao ni wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega katika safari za kisiasa za wenza wao mpaka kushika hatamu za madaraka. Wiki hii tunakuletea mfululizo wa makala kuhusu wenza wa marais katika eneo la Afrika Mashariki na leo tunakupakulia yote unayofaa kujua kumhusu mke wa rais wa Kenya .
Kwa muonekano, ni mwanamke mpole, mtaratibu na bila shaka kwa wanaomtazama huenda wakaafiki kuwa anastahili kuitwa jina analoitwa hasa wakati wa sherehe za kitaifa-Mama wa taifa. Lakini je Margaret Gakuo Kenyatta, ni nani hasa? na amekuwa na mchango gani katika taifa la Kenya na nje?
Margaret Wanjiru Gakuo alizaliwa tarehe 8 Aprili 1964 na Baba yake alikuwa Njuguna Gakuo, aliyekuwa Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la reli la Kenya raia wa Kenya na mama yake Magdalena alikuwa Mjerumani.
Alisomea masomo yake ya sekondari katika shule za Kianda School na St Andrew's Turi nchini Kenya na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini humo, ambako alipata shahada ya Elimu. Japo ni mkufunzi aliyesomea taaluma hiyo, hakuna ushahidi uliopo kwamba aliwahi kufundisha.
Kukutana na hatimaye kuoana na Bw Uhuru Kenyatta.
Kulingana na Rais Kenyatta, alifahamiana kwa mara ya kwanza na Bi Margret Gakuo walipokuwa wanafunzi katika shule moja ya sekondari. ''Nilipokutana naye hakuwa Mke wa rais. Alikuwa wa kawaida, msichana mzuri ajabu," alisema Bw Uhuru alipokuwa akizungumza na watumiaji wa mtandao wa Facebook, miaka 3 iliyopita.
''Nilifahamiana kwanza na kaka yake. Tulisoma wote katika shule moja ya sekondari na tukawa marafiki haraka na ni kupitia yeye ambapo niliweza kukutana na dada yake mdogo na tulianza mahusiano ambayo yalidumu kuanzia Shule ya sekondari hadi sasa. Namshukuru Mungu kwa hilo," alisema Uhuru.
Watoto
Bi Margret aliolewa na Bw Kenyatta katika Kanisa la Katoliki la Holy Family Basilica lililopo mjini Nairobi 1989 ambapo walifunga ndoa katika ibada iliyoongozwa na Maurice Kardinali Otunga na wamejaaliwa watoto watatu - Jomo, Jaba na Ngina.
Margret Kenyatta kama mke wa rais
Bi Magret Kenyatta Gakuo alikuwa Mke wa rais rasm kuanzia mwaka 2013, baada ya mume wake Bw Uhuru Kenyatta kuchaguliwa kuwa rais wa Kenya.
Tangu wakati huo Bi Margaret, amejitolea kwa vitendo kupigania maisha ya akina mama wa Kenya na watoto kupitia kampeni yake ya Beyond Zero.
Kampeni hii inalenga kutoa uelewa na kuchangisha fedha za kushughulikia afya ya akinamama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua pamoja na kuzuia maambukizi ya HIV ya mama hadi kwa mtoto.
Mwanzoni mwa Kampeni ya Beyond Zero Bi Margret Kenyatta alijitokeza binafsi kuanza mazoezi ya mbio za marathoni na baadaye kushiriki binafsi mbio hizo nchini Kenya na mbio za London marathon, kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa umma na dunia juu ya umuhimu wa kuchangia mpango huo.
Kufuatia juhudi zake, Bi Margaret Kenyatta aliweza kuchangisha mamilioni ya pesa na kuweza kununua magari ya kliniki (mobile Clinick), ambayo sasa yanawahudumia wanawake wajawazito na watoto hususan wenye matatizo ya dharura katika Kaunti mbali mbali nchini Kenya.
Kampeni hiyo imeweza kuokoa maisha ya akina mama na watoto na kumpatia umaarufu ndani na nje ya nchi, huku baadhi wakimuita mwanamke ''jasiri''.
Zaidi ya hayo Bi Margaret Kenyatta amekuwa akipaza sauti kwenye mikutano mbali mbali ya kitaifa na kimataifa kuhusiana na masuala ya mbali mbali ya kijamii, hususan yale yanayohusiana na maisha na hali bora kwa akina mama na watoto, elimu na uhifadhi wa wanyama pori pamoja na mazingira.
Kufuatia juhudi zake mwaka 2019 alianzisha kitengo maalum cha afya ya akina mama na watoto katika Hospitali ya Nakuru katikati mwa Kenya kilichopewa jina lake. Kitengo hicho hutoa huduma kwa watoto njiti na wanaozaliwa na matatizo mengine ya kiafya kwa wakazi wa Nakuru na maeneo mengine yanayozingira kaunti hiyo.
Bi Margret Kenyatta amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha Wakenya kubadili mtindo wa maisha ili kupambana na magonjwa yasiyoamkukiza kama vile saratani na kisukari , akisisitizia umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili kama njia ya kuepuka magonjwa hayo.
Mke huyu wa rais wa Kenya alitangazwa na Umoja wa Mataifa nchini Kenya, kama Mtu bora wa mwaka , kwa heshima iliyotokana na juhudi zake za kuboresha afya ya akinamama wajawazito na watoto nchini humo kupitia kampeni yake ya 'Beyond Zero'
Amekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kukomesha tatizo la fistula miongoni mwa wanawake wanaojifungua, huku akitoa wito wa kuwepo kwa juhudi za kudumu za kumaliza tatizo hilo akisema ''Mwanamke yeyote anayehangaika kutokana na fistula anapaswa kutibiwa mara moja na kurejea tena katika jamii '', alisema Bi Kenyatta mwezi Mei, 2021 baada ya kukutana na wanawake wanaohangishwa na Fistula kutoka Kitui, Baringo, Laikipia, Nakuru, Marsabit, Homa Bay na Nairobi.
Haiba na muonekano
Kwa Wakenya wengi Mke wa Rais Kenyatta Bi Margaret Kenyatta anatambuliwa kama ''Mama wa taifa'', kutokana na heshima anayopewa sio tu kwamba ni Mke wa rais, bali kutokana na haiba yake na matendo yake ya kiutu yanayoendana na heshima hiyo.
Muonekano wake umekuwa wenye mvuto, huku akitajwa na baadhi ya Wakenya na vyombo vya habari kama mama asiye na makuu na mnyenyekevu.
Unaweza pia kusoma:
Ni nadra kwa Bi Kenyatta kuzungumza na vyombo vya habari isipokuwa anapotaka kunadi shughuli za maendeleo yanayowahusu wanawake na watoto, afya na masuala mengine muhimu ya kijamii, kinyume na mtangulizi wake Bi Lucy Kibaki. Haiba yake ya utulivu imempatia mvuto miongoni mwa Wakenya wa tabaka mbali mbali.
Mtindo wake wa fasheni ya mavazi na nywele fupi zenye mvi zilizopamba kichwa chake umewavutia baadhi ya Wakenya hususan wasiopenda nywele bandia za kubandika:
''Yenyewe napenda sana vile mama wa taifa huvaa zile nguo za rangi ya maasai na shanga , kwa events, na hizo nywele zake nyeupe ako simple hana mambo mengi '', anasema Bi Shiro Wanjiku mkazi wa Nairobi na kuongeza kuwa ''Nikifika hiyo miaka yake nitakata nywele hivyo haki''.
Mtindo wake wa nguo hubadilika kulingana na matukio kuanzia Suti wakati wa sherehe rasmi za kitaifa, mavazi ya Kitenge na mchanganyiko wa mavazi ya kitamaduni ya kabila lake ya Gikuyu na na pia vazi la kitamaduni la Maasai.
Wachambuzi na wataalam wa fasheni nchini Kenya wamekuwa wakimpongeza kwa kuvaa nguo zilizobuniwa au kutengenezwa na wanamitindo Wakenya.
Kuna madai kuwa nyuma ya ukimya wake unaoonekana hadharani, Bi Margret Kenyatta, ana ushawishi mkubwa kuhusu baadhi ya masuala na maamuzi ya kitaifa anayoyachukua mume wake. Hatahivyo hakuna ushahidi unaodhihirisha madai haya.
Ni dhahiri hatahivyo kuwa Bi Margret Kenyatta kama mke wa rais, amechangia pakubwa katika uboreshaji wa afya ya mama na mtoto nchini Kenya kupitia kampeni yake ya ''Beyond Zero'' , historia ambayo haitasahaulika kuuhusu utawala wa mume wake Uhuru Kenyatta.