Rais Samia Suluhu aagiza kufanyiwa kazi malalamiko ya tozo

 


Rais Samia Suluhu Hassan ameguswa na malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu iliyoanza kutumika hivi karibuni na kuwaagiza mawaziri husika kutafuta suluhisho.

Hayo yamesemwa leo Julai 19 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupitia televisheni ya Channel Ten, akisema pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa na kikao na mawaziri husika ili kutafuta suluhisho.

“Tayari Mheshimiwa Rais ameshaguswa na jambo hili amesikia maoni ya Watanzania wote na amesema tuyafanyie kazi jambo hili,” amesema Waziri

Dk Mwigulu ameongeza kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na Waziri Mkuu. “Vilevile Waziri Mkuu ameitisha kikao kitakachofanyika kesho (Julai 20) kuendelea kupitia jambo hilo hilo.”

Amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuna mambo watakayoyafanyia kazi na mengine wataendelea kuwaelimisha wananchi.  

“Tumepokea maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa uelewa zaidi kwa maana ya uelimishaji zaidi ili kuwa na uelewa wa pamoja, ikiwa pamoja na viwango vinavyokatwa, yupi anayekatwa, ukataji wakati wa kutoa na mantiki ya jambo hili zima kwa ujumla,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa kuwa jambo hilo ni la kisheria zilizopitishwa na Bunge, utekelezaji wake utakuwa kwenye kanuni.

“Utekelezaji wake unaangukia kwenye kanuni za ambazo ni za Waziri na zinaangukia sehemu yangu Wizara ya Fedha na Wizara ya Tehama,” amesema.

Huku akitaka sheria ziheshimiwe, Waziri Mwigulu ameonya watu wanaopotosha jambo hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu.

“Wale wenye nia mbaya wanaopotosha kubadili maana kwa lengo la kupotosha maana halisi au kubadili dhana ya ya jambo lililokusudiwa wasifanye hivyo kwa mambo ambayo yana masilahi kwa Taifa letu. Mambo ya kisheria, sheria lazima ziheshimiwe na mambo ya kikanuni tuntaendelea kufafanua,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amesema Wizara yake imekuwa ikikusanya maoni kuhusu tozo hizo na itayafanyia kazi.

“Kama Wizara iliyoguswa na tozo hii tumekuwa tukikusanya maoni na ushauri na tumekuwa tukichakata takwimu tangu tozo hii ianzishwe.

“Wizara yangu itakupa ushirikiano kuhakikisha kwamba maelekezo ambayo tumepewa ili kuhakikisha kwamba amelekezo tuliyopewa na viongozi wetu na hata hapo kesho tutakapokutana katika kikao kingine tutakwenda kufikia mahali pazuri,” amesema.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post