Mpira una matokeo yanayoweza kubashirika kwa baadhi ya mechi kwa kuzingania namna timu zinazokutana zilivyojiandaa, uwezo wa timu, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na mipango mingine ya ndani na nje ya uwanja.
Lakini yapo matokeo mengine ambayo usingeweza kudhania yangetokea. Huko visiwani Zanzibar siku chache zilizopita, kuna mechi mbili ziliisha kwa matokeo ya kushangaza zaidi kwenye ligi ya mkoa wa Mjini Magharibi katika kuwania kupanda ligi daraja la kwanza visiwani humo.
Katika uwanja wa Mau B timu ya Umoja wa Mbuzini ilishinda jumla ya mabao 50-0, huku mchezo mwingine uliocheza katika uwanja wa Mau A timu ya Kundemba iliibuka na ushindi mnon wa mabao 46-0 dhidi ya Muungano Rangers.
Hakuna aliyeamini matokeo haya, yakionekana ni ya kupangwa na mamlaka za soka za Zanzibar zimechukua hatua ya kupiga faini na kuzishusha daraja timu zilizohusika na upangaji wa matokeo.
Arsenal aliwahi kufungwa 8-2 na Manchester United kwenye ligi kuu ya England msimu wa 2011/2012, Manchester City ilichapwa 8-1 na Middleborough mwaka 2008 na hivi karibuni tu msimu wa 2019/2020 Barcelona ilichapwa 8-2 na Buyern Munich kwenye mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya.
Matokeo haya si ya kutarajiwa na ni ya kushangazwa kiasi, lakini yapo matokeo mengine ya yanayoweza kukushangaza zaidi usivyo tarajia.
1: AS Adema 149 - 0 SO I'Emyrne (SOE)
Katika rekodi za dunia za kitabu cha Guiness, matokeo ya mechi kati ya AS Adema vs SOE yanashikilia rekodi ya dunia ya mechi yenye magoli ama mechi ya kipigo kikubwa zaidi cha magoli.
Ilikuwa mechi ya ligi kuu huko Madagascar iliyochezwa Oktoba 31, 2002 mjini Antananarivo. Kulikuwa na timu nne zinacheza mtoano katika hatua ya mwisho ya kumsaka bingwa wa ligi hiyo. Mchezo wa kwanza SOE ambayo ilikuwa bingwa mtetezi ilitoka sare ya 2-2 na DSA Antananarivo, katika mechi ambayo DSA walipata penati katika dakika ya mwisho ya mwisho, penati ambayo ililalamikiwa sana na SEO wakidai mwamuzi amewaonea.
Matokeo hayo ya sare yalimaanisha kwamba SOE wameutema ubingwa na hawana nafasi ya kuutetea ubingwa wao, sasa katika kuonesha kuchukizwa na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo uliopita wakaamua mechi iliyofuata wajifunge, na kweli wakajifunga magoli yote 149.
Walioshuhudia mchezo huo wanasema, kila mpira ulioanzishwa waliupiga golini kwao na kujifunga, huku wachezaji wa timu pinzani ya Adema wakisimama tu na kuwaangalia.
Mwisho wa siku Adema akatawazwa kuwa bingwa mpya huko shirikisho la soka la nchi hiyo (MFF) likimfungia kwa miaka 3 kocha wa SOE, Zaka Be na wachezaji watatu wakiongozwa na nahodha Manatranirina Andrianiaina pamoja na aliyekuwa nyota wa timu ya taifa ya Madagascar Mamisoa Razafindrakoto kwa kuonekana kuwa mstari wa mbele kwenye kupanga matokeo hayo.
Wachezaji wengine walionya, huku mwamuzi wa mchezo huo akionekana hana kosa lolote kwa kilichotokea uwanjani.
Huku mechi ikiedelea jukwaani kulikuwa na tafrani mashabiki wakitaka kurejeshewa pesa zao za tiketi kwa sababu ya kile kilichokuwa kinaendelea uwanjani, ilibidi serikali ya Madagascar kupitia wizara ya michezo iingilie kati kuokoa jahazi na kulifanyia marekebisho makubwa shirikisho la soka la nchi hiyo kuoka upangaji wa matokeo wa aina hiyo kujirudia.
2: Arbroath 36-0 Bon Accord
Kabla ya matokeo ya AS Adema 149 - 0 SO I'Emyrne (SOE) kwenye ligi ya Madagascar, matokeo ya mechi kati ya Arbroath na Bon Accord kwenye kombe la Scotland iliyopigwa Septemba 12, 1885 yalikuwa matokeo ya kushangaza zaidi yanayohusisha kipigo kikubwa cha magoli kwenye mchezo wa soka.
Arbroath iliingia kwenye mchezo huo ikiwa angalau ina uzoefu wa miaka 7 tangu kuanzishwa kwake wakati Bon Accord ilikuwa ina mwaka mmoja tu na inatajwa imeasisiwa kutoka kwenye timu ya mchezo wa raga.
Wachezaji wa Accord walikuwa na mchanganyiko wa jezi hasa kaptura na soksi, hawakuvaa inavyopaswa jambo lililoonyesha kwamba ni timu iliyotarajiwa kupata kipigo tu ilichokipata.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Accord walikuwa washapigwa mabao 15-0, kabla ya kipindi cha pili Arbroath kukamilisha kalamu ya mabao 21 na kumalizika kwa 36-0.
Bahati mbaya kwa golikipa wa Accord, Andrew Lornie ambaye ameingia kwenye rekodi za makipa waliofungwa magoli mengi zaidi kwneye mchezo mkubwa wa soka.
3: Dundee 35-0 Aberdeen Rovers
Wakati Arbroath ikiichapa 36-0 Bon Accord, kilometa 29, kwenye mji wa Dundee, kulikuwa na mchezo mwingine uliokuwa na matokeo ya kushangaza yenye magoli mengi na kuingia kwenye orodha ya mechi ya soka zenye matokeo ya ajabu zaidi.
Dundee Harp ilikuwa inacheza mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Aberdeen Rovers kwenye kombe la Scotland, mechi iliyoisha kwa Dundee kuichapa Aaberdeen mabao 35-0.
Jambo la kuvutia ni kwamba magoli yalifungwa kiasi kwamba mpaka watu wanasahau. Goli likifungwa wanaulizana ni la ngapi hilo. Kwa mfano muamuzi wa mchezo huo, hesabu zake zinaonyesha alirekodi mabao 37 ya Dundee, lakini katibu mkuu wa Dundee Harp akasema yeye amerekodi mabao 35.
Mwamuzi akasema ilikuwa ngumu sana kuhesabu kila bao kwa usahihi, kwa kuwa yalikuwa mengi mno uwahi kushuhudia kama mwamuzi wa kati.
Kwa mantiki hiyo, wazo la katibu mkuu wa Dundee Harp kwamba mabao yawe 35 likaridhiwa na Chama cha soka cha Scotland kikarekodi matokeo hayo ya 35-0.
4: Australia 31-0 na American Samoa
Ikiwa moja ya mechi zenye kuhusisha vipigo vikubwa zaidi kwenye soka, mechi hii ilikuwa muhimu kwa mabadiliko ya shsria nyingi za soka za leo hasa kwenye eneo la upangaji matokeo.
Baada ya mechi hii kumalizika Shirikisho la soka duniani likaanza kuongeza na kubadilisha sheria zake na kuweka adhabu kubwa kubwa ili kuzuia upangaji holela wa matokeo na kuua ladha ya mchezo wenyewe wa soka.
Ukweli kwamba mchezo huu ndio mchezo wenye magoli mengi zaidi uliohusisha timu za taifa na umetokea kwenye hatua za kufuzu kombe la dunia la mwaka 2002, ambapo ulipigwa nchini Australia
Aprili 11, 2001.
Katika mchezo huo nyota wa kimataifa wa Australia Archie Thompson alifunga mabao 13 peke yake, akivunja rekodi ya magoli mengi kufungwa na mchezaji mmoja katika mechi ya kimataifa. Huku timu ya Australia ikiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi wa timu ya taifa kwenye mchezo wa kimataifa.
5: Matokeo mengine ya hivi karibuni yaliyohusisha kapu kubwa la magoli
Desemba 2000 timu ya Carpati Mira ya Romania iliibanjua Avintul Dirlos mabao 41-0 lakini matokeo haya haya hayajawa rasmi kwa sababu mchezo huu haukuwa unatambulika na mamlaka za soka, ulikuwa mchezo wa ridhaa wa kujifurahisha licha ya timu zake kutambulika.
Machi 2012, timu ya mtaani ya Wheel Power F.C. ilishinda mabao 58-0 dhidi ya Nova 2010 F.C. na kuwa timu iliyopata ushindi mnono zaidi katika soka Uingereza, ikiipiku rekodi ya Illogan Reserves iliyoshinda mabao 55-0 dhidi ya Madron F.C. katika ligi ya Cornish Mining mwezi Novemba 2010.
May 2016 iliandikwa kalamu nyingine ya mabao kwenye soka kupitia mchezo mwingine kati ya Pelileo Sporting Club dhidi ya Indi Native, mchezo wa ligi daraja la tatu huko Ecuador. Mchezo huo ulimalizika kwa Pelileo kushinda mabao 44-1
Agosti 2, 2020, kwenye kombe la Poland katika ngazi ya mkoa huko Poznań, TPS II Winogrady iliichapa Big Show FC mabao 46-0, ushindi ulioweka rekodi katika mechi za soka zinazotambuliwa huko Poland.