Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai
Moshi. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameviagiza vyombo vya Dola likiwamo Jeshi la Polisi, kumhusisha katika kuandaa mashitaka ya watu watakaokamatwa kwa kupotosha kuhusu chanjo ya ugonjwa wa corona.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo mjini Moshi Agosti 7,2021 wakati wa uzinduzi utoaji chanjo kwa mkoa huo, huku akionya watumishi wa afya watakaofanya mzaha katika zoezi hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wale wote wanaopotosha vyombo vyetu viwe makini kufuatilia. Na yeyote mtakayemkamata amepotosha mchukueni. Wakati wa kuandaa mashitaka nihusisheni nitawasaidia”alisema mkuu huyo wa mkoa na kuongeza kuwa;-
Tutasaidiana kuandaa mashitaka dhidi ya huyo mtu kwa sababu ni mtu ambaye atakuwa amechezea maisha ya watu. Serikali iko serious (makini) kulinda maisha ya wananchi halafu mtu tu kwa ubababishaji wake anapotosha”
“Anaenda kwenye mitandao, anaenda kwenye pombe, kwenye baa anaanza kueleza mambo ambayo ni tofauti. Naomba sana vyombo vya ulinzi kwenye hili tufuatilie na tuwe makini. Maana hawa sio watu wema ni watu wabaya sana”
Mkuu huyo wa mkoa alitolea mfano wa mama yake mzazi ambaye alikuwa akisita kwenda kupata chanjo ya corona kutokana na upotoshaji wa chanjo lakini baada ya kumshawishi amekubali kuchanja na leo alienda kupata chanjo hiyo.
Kagaigai amesema mwitikio wa watu kujitokeza kupata chanjo ni mkubwa huku wananchi 10,300 kati ya 60,000 waliopangiwa kupata chanjo katika awamu ya kwanza wakipatiwa chanjo maeneo mbalimbali kuanzia Agosti 3 mwaka huu.
"Awamu ya kwanza tunatarajia kuchoma watu 60,000 ambapo hadi kufikia leo mkoa huu watu 10,300 wameshapata chanjo. Zoezi hili lichukuliwe kwa umakini mkubwa kwani ni suala la Kitaifa na lifanyike kwa haki ili iwafikie walengwa”
"Mwitikio ni mkubwa lakini nitoe wito kwa wataalam wa afya watakaofanya mzaha na viongozi wengine wa serikali niombe vyombo vya usalama viwe makini na fuatilieni hili maana ili suala ni la Kitaifa,"amesisitiza Kagaigai.
