Baadhi ya watanzania hii leo wamejitokeza katika vituo mbalimbali vilivyotengwa nchini humo kwa ajili ya kupata chanjo ya Covid19.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa chanjo hiyo kwa umma katika kipindi ambacho taifa hilo la Afrika Mashariki linakabiliwa na wimbi la tatu la janga la corona.
Tanzania, imepokea dozi milioni moja ya chanjo ya korona aina ya Johnson and Johnson kutoka Marekani kupitia mpango wa Covax, na mpaka sasa inalenga kufikia asilimia sitini ya wakazi wake.
Alipokuwa akipata chanjo yake kwa mara ya kwanza, rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema, kutokana na mahitaji ya chanjo hiyo kuwa makubwa, Tanzania imeagiza chanjo zaidi kupitia Umoja wa Afrika.
Kuanza kwa kampeni hii ya chanjo dhidi virusi vya korona, kunakuja wakati ambapo tayari maoni ya wananchi yamegawanyika hasa kuhusu utayari wa kuchanjwa na usalama wa chanjo hiyo.
Hali hii inatokana na dhana aliyoijenga aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ambapo alionekana kutokuwa na imani na chanjo hasa zile zinazotoka nchi za kigeni.
Kwa upande wake, rais Samia amejaribu kupambana na dhana hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kuongoza watanzania wengine katika kupata chanjo, huku akiwaasa raia kupuuza madai kwamba chanjo hiyo ina madhara.