WAZIRI BITEKO ATOA SIKU 60 LESENI ZISIZOFANYA KAZI KUFUTWA

 

Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza wakati Agosti 1, 2021 wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23 katika uwanja wa Zainab Telack Kijiji cha Butulwa Manispaa ya Shinyanga

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, akizungumza wakati Agosti 1, 2021 wakati Waziri wa Madini Doto Biteko akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga Agosti 1, 2021

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa katika banda la kampuni ya Barrick kwenye Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yaliyoanza Julai 23 katika uwanja wa Zainab Telack Kijiji cha Butulwa Manispaa ya Shinyanga.

***********************

Na. Steven Nyamiti – Shinyanga

Waziri wa Madini Doto Biteko, ametoa siku 60 za kufuta leseni za uchimbaji wa madini zilizohodhiwa na wawekezaji kwa muda mrefu bila kuzitumia.

Biteko amesema hayo Agosti 1, 2021 wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga  yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa Zainab Teleck kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.

Amesema, kumekuwepo na tatizo kwa baadhi ya wawekezaji wa madini kuhodhi leseni kwa muda mrefu na kutozitumia na pale yanapovumbuliwa madini na wachimbaji wadogo ndipo hujitokeza na kudai eneo hilo ni lao.

“Tutafuta leseni na mahakamani utakwenda, utatulipa kutoka mahakamani, kama una leseni endeleza leseni yako, hatutaki tuwasumbue wachimbaji wakubwa lakini vilevile wakubwa wasiwasumbue wachimbaji wadogo,’’ ameeleza Biteko.

Kufuatia hali hiyo, Biteko amesema wametoa siku 60 za kutaifisha leseni za uchimbaji wa madini zilizohodhiwa na wawekezaji kwa muda mrefu bila kuzitumia huku akibainisha kuwa Serikali imedhamiria kuinua Sekta ya Madini, pamoja na kumaliza migogoro yote ambayo hujitokeza baina ya wachimbaji wadogo na wakubwa.

“Naomba mfikishe salamu kwa wawekezaji wa madini ambao wana leseni za uchimbaji na hawazitumii, tumetoa siku 60 tu zianze kutumika, zaidi ya hapo tutazitaifisha na kutoza gharama ambazo Serikali imeingia kutokana kutolipiwa kodi kwa muda mrefu na kusababisha Serikali kukosa mapato na fedha hizi lazima zilipwe hatutakuwa na msalia mtume, hatutaki migogoro ya uchimbaji wa madini,’’ amesema Biteko.

“Tumeondoa kila aina ya kikwazo kilichokuwa kinawafanya watu watoroshe madini, tumeondoa kodi peke yake zaidi ya asilimia 23, tunaona watu kutoka Nje ya nchi Congo, Zambia na Msumbiji wanaleta madini kuja kuuza hapa, unashangaa kumuona Mtanzania na yeye anatorosha madini kupeleka mahali kwingine,” amesisitiza Biteko.

Aidha, amewataka wachimbaji wenye leseni walipe kodi na waepuke vitendo vya utoroshaji madini huku akibainisha kuwa atakayetorosha madini atakuwa anachoma madini kwa tochi, hivyo akikamatwa hatabaki salama na kuwataka wapeleke madini yote kwenye masoko.

“Tumefungua masoko, leo Tanzania tuna  masoko ya madini 39, tuna Vituo vya kuuza madini 50, na hata Shinyanga masoko yapo mengi, Mwaka 2019 tulifungua  soko la kwanza la madini na hili limetuletea faida kubwa, tuone fahali kulipa kodi, tuone fahali kupeleka madini kwenye masoko yetu, kama Wizara ya Madini tutaendelea kuwahudumia watanzania wanaohitaji kuchimba,’’ ameongeza Biteko

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula ameunga mkono  kauli ya Waziri Biteko kwa kutoa siku 60 kwa wawekezaji ambao wanamiliki leseni za uchimbaji madini na kutoziendeleza kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria, pamoja na kufidia fedha ambazo zilipaswa kulipwa kwa kipindi chote walichohodhi leseni hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati amesema maonesho hayo yamesaidia kuutatangaza Mkoa huo na kuonyesha fursa za biashara hasa katika sekta ya madini.

Pia, kama mkoa utaendelea kuboresha maonesho hayo na kuwaunganisha wafanyabiashara na wajasiriamali akiongeza kuwa maonesho hayo ni muhimu kwa sababu Mkoa wa Shinyanga una madini mengi na una madini ya pekee ya Almasi ambayo yanaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Kupitia maonesho haya washiriki wamepata fursa ya kutambulisha biashara zao, kuuza bidhaa na kujifunza teknolojia ya kisasa na kujua wapi wapate mitaji,’’ amesema Sengati.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) Hamza Tandiko amezishukuru Taasisi za kifedha kwa kuanza kuwapatia mikopo wachimbaji wa madini huku akiomba Serikali kupeleka umeme wenye nguvu ya kuendesha mitambo kwenye maeneo ya machimbo kwani umeme uliopo sasa ni kwa ajili ya mwanga tu.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Said Pamui ambao ni miongoni mwa wadhamini wakuu wa Maonesho hayo, amesema taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya CRDB zimeanza kuwezesha mikopo kwa vikundi vya wachimbaji wa madini na wajasiriamali hivyo kuwakaribisha kupata huduma katika Benki yao ambayo pia inatoa Bima za aina mbalimbali zitakazowasaidia wachimbaji.

Maonesho hayo yaliyokwenda kwa kauli mbiu ya Uwekezaji wa Madini na Viwanda Shinyanga kwa Uchumi Endelevu yaliyoanza Julai 23 na kufungwa Agosti 1 na Waziri wa Madini Doto Biteko.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post