Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
WANAWAKE wa Wilaya ya
Ngorongoro Mkoani Arusha, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutatua
migogoro ya ardhi Ngorongoro, ili kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake na
watoto ambao wamekuwa na hofu, wakiathirika na migogoro inayoendelea.
Mkurugenzi wa
shirika la utetezi wa wanawake na watoto la MIMUTIE, Rose Njilo
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha mashirika ya
utetezi wa wanawake na watoto Ngorongoro, amesema wanawake na watoto
wamekuwa wahanga wa migogoro inayoendelea.
Njilo amesema
wanawake wana imani kubwa na Rais Samia Suluhu kusaidia wanawake na
watoto Ngorongoro kwani wanakosa amani, watoto hawaendi shule, hakuna
huduma bora za afya.
Amesema mashirika ya
utetezi wa haki za wanawake na watoto, wana imani kubwa na Rais Samia
Suluhu kuwa anaweza kurejesha furaha na amani kwa wanawake na watoto wa
Ngorongoro na kwa kuingilia kati migogoro ya ardhi.
“Sisi tunaomba huduma
muhimu zitolewe Ngorongoro kama elimu, maji, afya na chakula, amani na
utulivu virejeshwe kwani kila mara migogoro imekuwa ikiibuliwa na
wanaopata shida ni wananawake na watoto,” amesema Njilo.
Amesema vijana wengi
wa jamii hiyo, wameondoa Ngorongoro na kwenda kufanya ulinzi katika nchi
jirani za Kenya na Uganda na wengine katika miji kama Dar es Saalam,
Arusha na Mwanza si kwa kupenda bali katika maeneo yao hakuna utulivu.
Mkazi wa Ngorongoro,
Mariam Kibore ameitaka serikali kutatua shida za wanawake wa watoto wa
Ngorongoro kwani wanaoshi maisha magumu, ikiwepo kukosa huduma muhmu.
“Tunaomba Serikali
itusaidie sisi wanawake, tuondokane na hofu kila siku hatujuwi kesho
itakuwaje, watoto hawasomi shule kwa amani,” amesema.
Wilaya ya Ngorongoro
imekuwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu Tarafa ya Loliondo na ndani
ya eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
