MASHABIKI wa Simba na Yanga wanahesabu siku tu kwa sasa kabla ya kushuhudia timu hizo zikishuka uwanjani kuvaana, huku nyota wa timu hizo, Fiston Mayele (Yanga) na Moses ’Le General’ Phiri (Simba) wakitajwa kuwa ndio walioshikilia ufunguo wa furaha ama huzuni katika pambano hilo.
Wakongwe hao wanavaana katika mechi ya 109 katika Ligi ya Bara tangu mwaka 1965 itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kocha wa zamani wa Biashara United, Amani Josiah akiwataja wachezaji hao na kumkingia kifua, kocha wa Simba Juma Mgunda, akisema jamaa anastahili kuaminiwa na uongozi na mashabiki wa timu hiyo na kupewa kandarasi ya kudumu.
Josiah alisema licha ya dabi, lakini Jumapili kutakuwa na vita ya Mayele na Phiri ambao wamekuwa wakizibeba timu hiyo na kwamba kama wakifanya vizuri ni wazi mashabiki wa timu ya mmojawapo watakuwa na furaha na wenzao watabaki na huzuni.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Tunduru Korosho alisema, mbali na nyota hao, lakini kuna wengine wa kuchungwa kama Clatous Chama na Feisal Salum wanaotarajiwa kutoa burudani huku shughuli pevu ikiwa kati ya Khalid Aucho na Sadio Kanoute.
“Nyota wa kuchungwa kwa pande zote ni Moses Phiri na Fiston Mayele na watakaoamua mechi hii ni walimu wa pande zote mbili hivyo naweka sare ya mabao kwa sababu ni mechi kubwa na nzuri yenye hisia kwa washabiki, wachezaji, mabenchi ya ufundi na viongozi,” alisema Josiah akisisitiza eneo la kiungo kwa timu zote ndio mhimili wa dabi hiyo ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu.