Taarifa iliyoshtua wengi ni juu ya wadhamini wakuu wa Yanga kampuni ya SportPesa kulalamika hatua ya klabu hiyo kuingia mkataba na wadhamini wengine wakuu maalum lakini bosi mmoja amefafanua.
Bosi mmoja wa juu wa Yanga amesema wameshangaa hatua ya wadhamini wao wakuu SportPesa wakilalamika juu ya uamuzi wao, na kwamba mapema waliwatafuta kwa nyakati tofauti na kuwaeleza juu ya nia yao hiyo.
Amesema kila hatua ya kuingia mkataba wa mechi sita na kampuni ya vifaa vya Kielektroniki ya Haier waliwajulisha SportPesa ingawa hawakuonyesha kukubaliana na mdhamini huyo.
"Tuliwatafuta mara nyingi kuanzia Novemba mwaka jana baada ya kufuzu hatua ya makundi, tukawaambia kimaandishi kwamba tunatafuta namna ya kuisaidia klabu kwa sababu kubwa wao hawataruhusiwa kikanuni," ameeleza bosi huyo.
"Wakatuambia tuwapelekee uthibitisho kwamba CAF hawairuhusu SportPesa, tukamtuma mtu wetu CAF akapewa uthibitisho huo na tukarudi na kuwasilisha kwao, hawakujibu, tukawakumbusha hawakujibu.
"Baada ya muda mwaka huu mapema tukawajulisha kwamba bado tunawatambua wao kuwa wadhamini wetu wakuu lakini tumepata mdhamini maalum ambaye hana mgongano nao wa kimaslahi ili tumtumie kwenye hizi mechi sita tu za hatua ya makundi.