Klabu ya Young Africans SC imethibitisha kufikia makubaliano ya kuachana na Kocha mkuu Nasreddine Nabi baada ya kocha huyo kuomba kutoongeza mkataba mpya.
Kupitia taarifa yake kwa umma klabu ya Yanga imesema mkataba wa Nabi na klabu hiyo umemalizika mwisho wa msimu huu na kubainisha kuwa ilikutana na Kocha Nabi kwa ajili ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya kocha huyo raia wa Tunisia aliomba kuondoka ili akapate changamoto mpya.
“Akiwa Kocha Mkuu wa Young Africans Sports Club, Nabi amefanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya NBC, mataji mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam, mataji mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha timu yetu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF.” imesema taarifa hiyo.
“Uongozi wa Young Africans Sports Club unamshukuru Kocha Nabi kwa mchango wake katika kipindi chote alichofanya kazi kwenye timu yetu na unamtakia kila la kheri katika safari yake.”
“Aidha, Uongozi wa Young Africans Sports Club umeanza mchakato wa kumpata Kocha mpya atakayechukua nafasi ya Kocha Nasreddine Nabi.”
#KitengeSports