15 mbaroni wakituhumiwa kujiunganishia bomba la mafuta bandarini Dar


Dar es Salaam. Watu 15 wamekamatwa kwa mahojiano wakidaiwa kujiunganishia mabomba kutoka katika mtambo wa mita za upimaji wa mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na kuiba mafuta.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya kushtukiza katika mtambo huo iliyofanywa leo Jumatatu Juni 13, 2021 na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

Katika ziara hiyo, Makalla aliambatana na mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na usalama wakiongozwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Mwananchi Digital imejionea namna watuhumiwa hao walivyochimba kisima na kuunganisha bomba linalopita chini ya ardhi na kwenye makazi ya watu hadi katika bomba kuu la kupitishia mafuta kutoka bandarini hadi katika mtambo huo.

Makalla amesema amepokea maelezo ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa namna magari ya kubebea mchanga na kokoto yalivyogeuzwa kuwa matanki ya kubebea mafuta ya wizi.

“Ndani  wanaweka tenki la mafuta halafu kwa juu wanafunika na kokoto au mchanga ili isijulikane walichobeba kwa ndani.”

“Nipongeze kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Kigamboni ikiongozwa na mkuu wa wilaya kwa kazi kubwa waliyofanya hadi kufanikisha zoezi hili la kukamata watuhumiwa 15 na bado wanaendelea na uchunguzi na watakamatwa wengine zaidi,” amesema.

“Iwe ndani ya taasisi zetu za Serikali au nje, kama tunavyofanya operesheni za ujambazi basi jambo hili tulifanyie operesheni ya aina yake Ili kukomesha mtandao huu. Tumeshuhudia namna ambavyo mtu kajenga nyumba yake kaweka kamera za ulinzi na karakarana na kujiunganishia mtambo wa mafuta, huu ni uhujumu uchumi,” amesema.

Naye Muliro amesema jambo hilo lilishafika katika mamlaka za juu za Serikali na ikaundwa tume maalum kuchunguza na uchunguzi utakapokamilika watalitolea taarifa kamili.


Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post