Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amefanya ziara ya kushtukiza katika mtambo wa kupima mafuta Bandari ya Dar es Salaam uliopo Kigamboni na kubaini wizi wa mafuta unaofanywa na baadhi ya wananchi.
Amefanya ziara hiyo leo Jumatatu Juni 14, 2021 akiambatana na mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama akiwemo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ameamua kufanya ziara hiyo baada ya malalamiko ya wafanyabiashara wanaoagiza mafuta kupewa mafuta pungufu na yale waliyoagiza na kulipia.
“Tumejiridhisha na kubainisha kwamba upo wizi wa mafuta, watu wamejiunganishia miundombinu na kuiba mafuta na kuyauza kinyemela,” amesema.
Katika hatua nyingine, Makalla ameitisha kikao kati yake, waagizaji wote wa mafuta, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Uagizaji Mafuta Pamoja Tanzania (PBPA) kitakachofanyika Juni 21, 2021.
Amesema haiwezekani watu wa nje wakajiunganishia mitambo ya kuiba mafuta na kuyauza bila wenye mitambo mikubwa ambao ni TPA kujua.
“Nimeshasikiliza upande mmoja ambao ni TPA ila sijaridhishwa na majibu yao, inawezekanaje mtu ajiunganishie bomba la mafuta halafu wenye mtambo wasijue.”
“Jumatatu ijayo (Juni 21) saa tatu asubuhi tutakuwa na kikao pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ili tujiridhishe kwa nini wizi huu umetokea, tuone uzembe uko wapi lakini pia tuone hatua za kuchukua ili jambo hili lisijirudie tena,” amesema Makalla.