Mfungwa aliyetoroka gerezani akamatwa mkoani Iringa



Iringa. Jeshi la polisi Mkoa wa Iringa limemkamata Dennis Ngumbi aliyetoroka gerezani na watuhumiwa wengine 23 kwa tuhuma za makosa mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 14, 2021 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Juma Bwire amesema mfungwa huyo alitoroka katika gereza la Isupilo lililopo wilayani Mufindi.

Bwire amesema mfungwa huyo alikuwa akitumikia kifungo cha miaka minne jela na alikamatwa saa 5 asubuhi katika kijiji cha Igowole  wilayani Mufindi.

"Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni maalum ambayo ni endelevu anayolenga kutokomeza uhalifu na tumekamata watuhumiwa 23 kwa makosa mbalimbali yakiwemo kumiliki silaha bila kibali,” amesema Bwire.

Amebainisha kuwa katika kituo cha Igowole wilayani Mufindi watuhumiwa Ernesto Muheme (67),  Hamis Ngoze (55) na Lucas Muhume (50)  walisalimisha silaha tatu aina ya gobole.

Amesema katika maeneo ya Mwantingo kata ya KIhesa polisi walimkamata, Abunuel Mgaya (30) mkazi wa Mwanyingo akiwa na vitu mbalimbali vya wizi.

Kamanda huyo amewataka wananchi katika maeneo mbalimbali kufika kituo cha polisi kutambua mali zao.


Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post