Chadema yataka ‘kodi ya katiba mpya’


Dar es Salaam. Siku mbili baada ya bajeti ya Serikali kuwasilishwa bungeni jijini Dodoma, Chadema imeibuka na hoja ya Katiba mpya ikisema wananchi wako tayari kugharimia mchakato wa kuandika katiba yao hata kwa Serikali kubuni kodi maalumu ya Katiba.

Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika jana aliichambua bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni Juni 10 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, akigusia mambo mbalimbali ikiwemo kodi mpya ya laini za simu na kodi ya majengo kwa njia ya luku, alizosema hazina tija kuliko kile alichokiita ‘kodi ya katiba’.

Mnyika alisema chama chake kinataka masuala ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi yaingizwe kwenye bajeti ya Serikali, kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi wake.Alisema katiba mpya ndiyo mradi muhimu kwa Taifa kwa sasa, kwa sababu itajenga misingi ya ujenzi wa Taifa bora kwa miaka zaidi ya 50 ijayo.

“Jambo la kipaumbele kuliko yote ni kufikiria kuandika katiba mpya kwa sababu ndiyo mchakato muhimu kwa maendeleo ya nchi,” alisema Mnyika. Mwanasiasa huyo aliwataka Watanzania kujadili kuhusu suala la katiba mpya kama kipaumbele muhimu ambacho Serikali yao inapaswa kukifanyia kazi katika bajeti ya mwaka huu kwa sababu wameitafuta kwa miaka mingi.

Kuhusu suala la gharama za kuendesha mchakato huo, Mnyika alisema wananchi wako tayari kutozwa “kodi ya katiba mpya” ili kufanikisha mchakato wa kupata katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.

“Najua Serikali itatuambia kwamba hawana fedha za kuanzisha mchakato wa katiba mpya, watuambie. Sisi tuko tayari kulipa kodi ya katiba mpya badala ya hizi kodi walizozianzisha za laini ya simu na kodi ya majengo kwa kupitia Luku,” alisema.


Aliitaka Serikali kuziondoa kodi za laini ya simu na ile ya majengo itakayolipwa kupitia Luku, kwa madai kwamba itawaumiza wananchi hasa wapangaji ambao watalazimika kulipia majengo yasiyokuwa yao.

Mnyika alisisitiza kwamba ni muhimu mradi wa katiba mpya kuingizwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022, kwa sababu mchakato usipoanza mwaka huu, katiba mpya itachelewa kupatikana.

Alisema mchakato wa katiba mpya utahusisha pia mabadiliko ya sheria nyingi ili ziendane na katiba hiyo, hivyo, ni muhimu kwa suala hilo kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu, ili katiba mpya ipatikane kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wito kwa wabunge

Mnyika aliwataka wabunge kutafakari umuhimu wa suala hilo kabla ya kupitisha bajeti iliyowasilishwa na Serikali kwa sababu wananchi wanataka katiba na wao kama wabunge wana wajibu wa kufanya maamuzi kwa niaba ya wananchi.

Tangu Rais Samia alipoapishwa, Machi 19, Chadema imekuja na ajenda yake ya kupigania suala la katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, na kwamba hawatashiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao kama masuala hayo hayatafanyiwa kazi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anaendelea na mikutano yake ya ndani katika mikoa mbalimbali, huku moja ya ajenda zake kubwa ni kuhamasisha vuguvugu la kupata katiba mpya.

Mei 31 akiwa Musoma mkoani Mara, Mbowe alisema chama hicho kinaendelea kushikilia msimamo wake wa kutoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 bila kuwapo kwa Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi itakayosimamia uchaguzi huo.

Mbowe alisema chama hicho kinaangalia namna ambavyo kitashinikiza kupatikana kwa katiba mpya ikibidi hata kwa njia ya maandamano ya nchi nzima kuanzia makao makuu ya kata, jimbo, mkoa na Taifa.

“Tunaposema hatutashiriki uchaguzi mkuu hadi tuwe na katiba mpya na tume huru, sio kwamba tunataka ushindi wa mezani, hapana. Tunataka mipango mizuri ili rais ajaye, awe wa Chadema au chama kingine, afanye kazi kwa maslahi ya Watanzania wote,” alisema.

Mchakato wa kuandika katiba mpya ulianza mwaka 2012 baada ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Tume ya Warioba ilifanikiwa kutengeneza rasimu ya katiba ambayo ilikubalika na makundi mbalimbali, hata hivyo, ilifanyiwa mabadiliko makubwa mpaka kupatikana kwa katiba inayopendekezwa, mwaka 2014.

Licha ya kupitishwa na Bunge, Katiba Pendekezwa haijakubalika na wadau wengi, jambo linaloibua mjadala wa wapi mchakato wa katiba mpya uanzie.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post