Gazeti la Daily Apple laongeza uzalishaji baada ya kushikiliwa wahariri wake
Gazeti la kila siku la Apple Daily la Hong Kong leo limeongeza uzalishaji mara tano zaidi ya idadi ya kawaida hadi nakala 500,000 huku kukishuhudiwa mistari mirefu ya watu wanaonunua gazeti hilo ikiwa ni sehemu ya kuonyesha uungaji wao mkono wa uhuru wa kujieleza unaokabiliwa na wakati mgumu. Hatua hii inakuja siku moja baada ya polisi kuwakamata wahariri watano waandamizi pamoja na watendaji wakuu wa gazeti hilo.Hatua ya kuvamiwa kwa ofisi za gazeti hilo pamoja na kukamatwa kwa mali zake za thamani ya dola milioni 2.3 ni ya mwanzo katika utekelezwaji wa sheria tata ya usalama wa taifa dhidi ya vyombo vya habari na ishara ya karibuni kabisa ya kuzuia uhuru wa watu wa jiji hilo lisilo na mamlaka kamili. Kulingana na polisi wahariri hao walikamatwa kwa madai ya kula njama na raia wa kigeni na kuhatarisha usalama wa taifa. Waziri wa usalama hapo jana aliwaonya waandishi wengine kujitenga na wahariri hao wa gazeti la Apple wanaochunguzwa.