Wapiga kura nchini Iran watamchagua rais mpya Ijumaa wiki hii, huku mhafidhina wa msimamo mkali Ebrahim Raisi akitarajiwa kumrithi Hassan Rouhani mwenye siasa za wastani.
Hii ni baada ya wagombea kadhaa kufungiwa kushiriki. Uchaguzi huo unakuja katika wakati ambao nchi hiyo inayokabiliwa na mfumko wa bei ipo kwenye mazungumzo na madola yenye nguvu kwa ajili ya kuufufua muafaka wa nyuklia wa 2015 na hamu ya kuukamilisha utawala uliowekewa vikwazo vikali vya Marekani.
Mamlaka kamili nchini Iran tangu mapinduzi ya mwaka wa 1979 yapo mikononi mwa Kiongozi wa juu kabisa, Ayatollah Ali Khamenei, lakini rais ana ushawishi mkubwa kuhusu masuala muhimu kuanzia sera ya kiviwanda hadi mambo ya kigeni.
Mafanikio ya kihistoria ya mihula miwili ya miaka minne kila muhula ya Rouhani, ambayo inaruhusiwa kikatiba, ni muafaka wa nyuklia ambao Tehran ilikubali kupunguza shughuli zake za nyuklia ili nayo iondolewe vikwazo vya kimataifa.
