Jinsi bilionea wa IPTL alivyoianza safari ya maisha ya mahabusu- 1






Jumanne ya Juni 16, mwaka huu wa 2021, ilikuwa ni siku nyingine ya pekee katika historia ya maisha ya mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi baada ya kurejea uraiani kutoka mahabusu.

Siku hiyo ilikuwa ni hitimisho la safari ya siku 1,458, takribani miaka minne ya kuishi mahabusu katika magereza mbalimbali, alikokuwa akihifadhiwa yeye na wenzake wawili, kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka yasiyodhaminika ya utakatishaji fedha haramu.

Katika kesi hiyo ya uhujumu Uchumi namba 17 ya mwaka 2017, yeye na wenzake, mfanyabiashara maarufu na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni hiyo ya IPTL, James Buchard Rugemalira, na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni hiyo Joseph Makandege walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 12.

Mashtaka hayo yaliyotokana na kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya pesa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa katika Benki Kuu kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za uwekezaji baina ya IPTL na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lililopinga malipo hayo kuwa yalikuwa makubwa.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na pande hizo mbili kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo hayo kusubiri utatuzi wa mgogoro huo kuhusiana na kiasi ambacho Tanesco ilipaswa kukilipa.

Mashtaka hayo aliyokuwa akikabiliwa nayo Seth pamoja na wenzake ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya dola za Kimarekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Hata hivyo, bilionea huyo alirejea uraiani tena baada ya kujitia hatiani mwenyewe, kwa kukiri mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, kwa utaratibu wa makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ambapo alihukumiwa kulipa fidia ya Sh26.9 bilioni, kama walivyokubaliana na DPP.

Hivyo wakati Seth akitoka mahabusu, wenzake hao wanaendelea na maisha ya mahabusu wakisubiri kusikilizwa na kuamriwa kwa mashtaka yanayowakabili kwa kuwa hawajataka kufanya majadiliano na DPP katika kumaliza kesi hiyo inayowakabili.

Lakini, safari hiyo ilianzaje na lini na mwenendo wa kesi hiyo kwa upande wake ulikuwaje kabla ya hitimisho la safari hiyo. Fuatana nasi katika simulizi hii tukupitishe kwa muhtasari katika safari yake hiyo ya maisha ya gerezani, hususan mwenendo wa kesi hiyo mahakamani kwa upande wake.

Mwanzo wa safari ya maisha ya mahabusu

Safari ya maisha ya Seth mahabusu ilianza Juni 19, 2017, alipopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar e Salaam, Kisutu, baada ya kutiwa mbaroni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Julius Nyerere (JNIA), akijiandaa kusafiri nje ya nchi na mkewe.

Siku hiyo Seth na Rugemalira walifikishwa mahakamani hapo saa 8.30 mchana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakiwa chini ya ulinzi. Baada ya kushushwa kwenye gari waliamuriwa kuchuchumaa kabla ya kuingizwa mahabusu kusubiri kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yao.

Muda mfupi baadaye walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka sita kwa pamoja, yaani kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara ya jumla ya Sh358 bilioni.

Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, wakati huo akiwasomea mashtaka alidai kuwa walitenda makosa hayo kwa nyakati na mahali tofauti kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 ndani na nje ya nchi kama vile jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Seth ni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), iliyodai kuinunua IPTL kutoka kwa wamiliki wa awali, Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad iliyokuwa ikimiliki hisa asilimia 70 na Rugemarila, ambaye ni mkurugenzi wa VIP Engineering and Marketing, aliyekuwa akimiliki asilimia 30.

Lakini, Mechmar ilikana kutambua mchakato wa ununuzi wa hisa za kampuni hiyo ikidai kuwa haukuwa halali kwa kuwa ulikiuka mkataba wa makubaliano wa wanahisa hao, kwani ulifanyika bila ridhaa ya Bodi ya wakurugenzi kama ilivyokuwa katika mkataba huo.

Kufuatia hatua hiyo ya PAP kuinunua IPTL, ilijimilikisha mali zote za IPTL, ikiwemo Akaunti ya Tegeta Escrow pamoja na pesa zote zilizokuwemo ambazo zilikuwa zikiwekwa na Tanesco kama malipo ya gharama za uwekezaji kusubiri kutatuliwa kwa mgogoro baina yake na IPTL.

Kadushi alidai katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao, wakiwa si watumishi wa umma waliunda mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida. Seth alikuwa anadaiwa kuwa alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni na kuonyesha kuwa ni Mtanzania anayeishi Mtaa wa Mrikau, Kitalu Namba 887, Masaki jijini Dar es Salaam, uongo anaotuhumiwa kuufanya Oktoba 10, 2011.

Pia alidaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajili wa kampuni, Seka Kasera kwa nia ya kuonyesha kuwa yeye ni Mtanzania na anaishi mtaa huo.

Washtakiwa wote walidaiwa kujipatia kwa ulaghai kutoka Benki Kuu (BoT) dola 22,198,544.60 za Kimarekani na Sh309,461,158.27 za Kitanzania kati ya Novemba 28, 29 mwaka 2011 na Januari 23, 2014 wakiwa makao makuu ya benki ya Stanbic, Kinondoni na benki ya Mkombozi, tawi la St Joseph.

Vilevile wote walidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha wakidaiwa kwa tukio lililotokea Novemba 29, 2013 katika tawi la Kati la benki ya Stanbic.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi aliwaeleza kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashtaka hayo, na kwamba watasikilizwa na Mahakama Kuu isipokuwa kama DPP atatoa kibali kwa mahakama hiuo kuisikiliza kesi hiyo.

Kwa kuwa DPP hakuwa ametoa kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, ingawa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili yote yalikuwa yana dhamana, lakini mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kutoa au kusikiliza maombi yao ya dhamana, badala yake walipaswa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

Hata hivyo, licha ya msimamo huo wa kisheria, wakili wa utetezi, Respicius Didas aliomba mahakama iwape wateja wake dhamana akisema mashtaka yao yanadhaminika.

Wakili Kadushi alipinga maombi hayo akieleza kuwa mamlaka hayo ya kutoa dhamana ni ya Mahakama Kuu na kwamba, ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote baada ya kusomewa mashtaka hayo.

Wakili Kadushi alieleza kuwa mazingira pekee ambayo yangeifanya mahakama hiyo isikilize maombi hayo ni pale DPP anapotoa kibali maalumu cha kuipa mamlaka hayo mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 3 na akaamuru washtakiwa hao wapelekwe mahabusu hadi tarehe hiyo ya kesi.

Washtakiwa hao walipelekwa katika mahabusu ya gereza la Keko na huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya mahabusu wa Seth na mwenzake wakati wakisubiri kuwasilisha maombi ya dhamana yao Mahakama Kuu.

Kesi hiyo ilikuwa ni moja ya kesi kubwa na yenye kuvuta hisia za umma pamoja na mambo mengine kutokana na asili ya mashtaka yake, kwani itakumbukwa kashfa hiyo iliibua mjadala mkali bungeni mwaka 2014.

Katika mjadala huo, hatimaye Bunge lilifikia maazimio kwamba wote waliohusika na kashfa hiyo wachukuliwe hatua za kisheria, kwani pesa hizo zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilikuwemo za Serikali na kwamba zilichotwa isivyo halali.

Ripoti ya uchunguzi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, ilieleza kuwa sehemu ya pesa hizo zilizochotwa katika akaunti hiyo ziligawiwa, katika mazingira tata kwa wanasiasa, viongozi wa Serikali, baadhi ya majaji na viongozi wa dini.

Kama mashtaka yao yalikuwa yanadhaminika, je, walichukua hatua gani kusaka dhamana na kwa nini waliendelea kusota mahabusu hadi Seth alipotoka kwa utaratibu huo na kuwaacha wenzake wakisota mahabusu? Usikose sehemu ya pili kesho.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post