Dodoma. Jina la Rais Samia Suluhu Hassan limekuwa halibanduki kinywani mwa wabunge wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali Kuu ya mwaka 2021/22, bila kujali vyama wanavyoviwakilisha.
Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Juni 10 mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, ambapo anaomba Bunge kuidhinisha Sh36.3 trilioni katika mwaka 2021/22.
Wabunge watahitimisha mjadala huo Jumanne Juni 22 mwaka huu ambapo watapiga kura za uamuzi za wazi kwa kuitwa mbunge mmoja mmoja bungeni.
Akichangia mjadala wa makadirio hayo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Munde Abdallah alisema Tanzania imepata Rais msikivu ambaye amesikiliza vilio vya Watanzania na kuweka vitu vingi katika bajeti yake.
“Nawapongeza pia mawaziri kwa kweli wamekuwa sikivu, wanyenyekevu, wamechukua mambo yetu huku bungeni na kwenda kukaa na amiri jeshi mkuu ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke na kutuletea bajeti nzuri ambayo mimi nikiwa ni bajeti yangu ya 11 tangu nikiwa mbunge nimeiona bajeti ya kipekee,” alisema Munde.
Alisema bajeti hiyo imepanua wigo wa kodi, lakini pia imeleta kodi za kisayansi ambazo hazimuumizi moja kwa moja mwananchi kwasababu atazilipa bila kujisikia.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alisema bajeti hiyo ya kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita ni nzuri sana.
“Nimpongeze Rais (Samia) hii ni bajeti yake ya kwanza kwa Serikali ya awamu ya sita na ni bajeti nzuri sana katika historia ya bajeti zetu, ni nzuri sana na kama bajeti yake ya kwanza imefanyika hivi, nadhani kama tukimpa bajeti kama 10 hivi nchi yetu itakwenda vizuri zaidi,” alisema.
Amour Khamis Mbarouk (Tumbe-CCM) alimpongeza Rais Samia kwa kuwaletea bajeti hiyo ambayo imesababisha hata walio wachache bungeni kuifurahia.