Tahadhari viashiria vya corona mpya yatolewa

 


Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitoa tahadhari ya viashiria vya wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19, imeagiza utamaduni wa uvaaji barakoa, unawaji mikono na matumizi ya vitakasa mikono urudishwe katika maeneo yote.

Waganga wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi wengine wa sekta za umma na binafsi wamehimizwa kusimamia maagizo hayo.

Agizo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema wananchi wahakikishe wanaepuka misongamano isiyo ya lazima, ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri, misiba, makanisani, kwenye mipira na kuzingatia kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka kwa mtu mmoja kwa mwingine.

Aliagiza wananchi wahakikishe wanafanya mazoezi mara kwa mara, wanazingatia lishe bora, walio katika hatari wakiwemo wenye umri mkubwa, magonjwa sugu na unene kupita kiasi wachukue tahadhari na kuwahi matibabu wanapohisi kuwa na ugonjwa.

Dk Subi aliagiza uvaaji wa barakoa safi na salama ya kutengeneza mwenyewe au iliyozalishwa na wazalishaji wa ndani waliothibitishwa.

“Niwaombe wataalamu wa afya kutoa elimu kwa jamii juu ya uvaaji sahihi wa barakoa na zivaliwe katika maeneo yote yenye misongamano ya watu,” alisema Dk Subi na kuongeza:

“Wizara inawakumbusha wananchi wote kutopuuza ugonjwa huu wa Covid-19. Wizara imeanza kuona viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la mlipuko wa ugonjwa huu katika nchi yetu, hii ni kutokana na taarifa za ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa huu zinazofanywa na wizara na mwingiliano kati ya watu wetu na mataifa mengine kutokana na shughuli za kijamii na kiuchumi.”

Alisema idadi ya wagonjwa wanaokutwa na virusi vya corona Afrika imekuwa ikiongezeka kwa wiki 5 mfululizo, ikiwemo nchi jirani zinazoizunguka Tanzania na kwamba maambukizi yameendelea kuongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa kwa wimbi la pili.

Dk Subi aliwakumbusha wakuu wa mikoa, wilaya, viongozi wa wizara, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wote wa dini na kijamii kuchukua hatua za kiuongozi katika kuelimisha, kuratibu na kusimamia jamii katika kuchukua tahadhari.

Aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya, maofisa afya wanaotoa huduma mipakani kuendelea kuimarisha udhibiti wa magonjwa katika maeneo yao.

Corona ilivyoingia

Machi 16, 2020 Serikali ilitangaza uwepo wa ugonjwa huo baada ya mkazi wa Arusha, Isabela Mwampamba kugundulika kuwa na virusi hivyo akitokea nchini Ubelgiji, Machi 15, 2020.

Msafiri huyo aliondoka Tanzania Machi 3, 2020 ambapo kati ya tarehe 5-13 Machi alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji.

Machi 17, 2020, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitangaza kuzuia mikusanyiko na kufungwa kwa shule zote za awali, msingi na sekondari kwa siku 30 kuanzia siku hiyo baada ya kuthibitika kuwepo kwa mgonjwa wa corona hapa nchini.

Virusi hivyo vya corona viligundulika kwa mara ya kwanza katika jimbo la Wuhan nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

tangu wakati huo virusi hivyo vimekuwa vikisambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali ambapo hivi sasa India ndiyo inayotajwa kuathirika zaidi na wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post