Jumanne Juni 15, 2021 Afrika ilishtushwa na taarifa za kifo cha Rais wa kwanza wa Zambia Dk Kenneth Kaunda baada ya kulazwa hospitali akiuguwa homa ya mapafu. Amefariki akiwa na umri wa miaka 97.
Dk Kaunda maarufu KK ameaga dunia akiacha swali ni kwa umbali gani alikuwa na ushawishi kwa mwandani wake, Rais wa Tanganyika na baadaye Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na kurejea mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini humo 1992?
Mfumo wa vyama vingi Tanzania ulifutwa kufuatia marekebisho ya katiba ya mpito 1965 mwaka mmoja baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo kuwa na chama kimoja tu,Tanganyika African National Union (TANU).
1972, miaka minane baada ya uhuru, Zambia ikafuata njia hiyo hiyo na kubakia chama kimoja tu, chama tawala United National People´s Union (UNIP) Ulikuwa mtindo uliofuatwa takriban na mataifa mengi barani Afrika.
Baada ya miongo kadhaa, wimbi la mabadiliko ya kisiasa duniani mapema miaka ya 1990, lililofuatia kuanguka ukuta wa Berlin 1989 na kuporomoka mfumo wa kikoministi katika Muungano wa Jamhuri za Kisovieti (Urusi ya zamani) na nchi za Ulaya mashariki, liliitikisa dunia. Ulikuwa mwisho wa ile enzi ya mvutano wa miongo kadhaa katika siasa za dunia kati ya kambi za Mashariki na Magharibi na Afrika haikusalimika na mabadiiko hayo.
Kaunda kukubali kushindwa na upinzani
Miaka 19 baadae, 1990 Zambia ikarudi tena katika mfumo wa vyama vingi na kuwa na uchaguzi mwaka uliofuata. Chama cha UNIP kilikabiliwa na ushindani mkali wa chama cha upinzani Movement fo Multi-Party Democracy (MMD). Dk Kaunda akashindwa na mgombea wa MMD na Kiongozi wa chama hicho Frederick Chiluba, ambacho kilifanikiwa pia kuwa na wingi bungeni. MMD kikijulikana pia kama `Matumaini Mapya`.
Kushindwa kwa Kaunda kulitokea katika wakati ambao Mwalimu Nyerere alikuwa ameshastaafu Urais miaka mitano kabla na kumuachia mrithi wake Ali Hassan Mwinyi. Hata hivyo bado alikuwa na ushawishi katika siasa za taifa hilo. Wadadisi wanaamini baada ya Kaunda kuamua Zambia irudi katika mfumo wa vyama vingi, uamuzi wake ulikuwa na ushawishi kwa Mwalimu Nyerere, kwani kauli ya Mwalimu kwamba wakati umewadia kwa Tanzania kufikiria kurudisha mfumo huo, aliitoa mjini Lusaka Zambia.
Nyerere alikuwa ni nguvu iliyo lisukuma bunge la chama chake tawala cha Mapinduzi (CCM) alicho kiasisi, lirekebishe kifungu cha katiba 1992 na kuurudisha mfumo wa vyama vingi. 1995 ukafafanyika chaguzi wa kwanza ambapo CCM iliibuka mshindi na kubakia madarakani kinyume na yalioikuta UNIP.
Pamoja na hayo Dk Kaunda alipongezwa kwa kuyakubali matokeo aliposhindwa na Chiluba. Kuna dhana ya kwamba alipojaribu kurudi tena katika uchaguzi wa 1996 kabla ya Chiluba kumzuwia kwa kuibadili katiba na kuwekwa kifungu kinachomtaka Rais wa Zambia wazazi wake wawe wamezaliwa nchini humo.
Wazazi wa Kaunda walizaliwa Nyasaland (Malawi), ambapo wakati huo, kukiwa na kile kilichoitwa Shirikisho la Nyasaland lililozijumisha nchi tatu, koloni la Nyasaland na himaya za Uingereza za Rhodesia Kusini na Rhodesia.Liliundwa 1953 na kuvunjika 1963.
Chiluba alimuweka ndani mtangulizi wake aliyegeuka kuwa adui na Mwalimu Nyerere alisaidia rafiki yake kuachiwa.
Kwa upande mwengine huenda mabadiliko nchini Zambia yalimshawishi kwa njia moja au nyengine Rais wa Malawi Dr Hastings Kamuzu Banda (Ngwazi) vile vile akubali matokeo aliposhindwa katika uchaguzi 1994 na mpinzani wake Bakili Muluzi. Banda aliyekuwa dikteta aliwashangaza wengi.
Usuhuba wa Kaunda na Nyerere
Dk Kaunda na Mwalimu Nyerere walishirikiana kisiasa kwa karibu na kuwa takriban na dira inayofanana. Wote waliamini juu ya Usoshalisti, huku falsafa yao ikitafautiana kwa majina pekee. Nyerere aliita sera yake kuwa ya `Ujamaa` na Kaunda ´Utu`. Walikuwa na mshikamano katika siasa za bara la Afrika na kimataifa, kuanzia umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote.
Viongozi hao walikuwa na sahibu wao mwengine wa chanda na pete, Rais wa zamani wa Uganda Milton Obote. Obote aliyevutiwa na falsafa ya Usoshalisti alipewa hifadhi na kuishi uhamishoni nchini Tanzania baada ya kupibduliwa na mwanajeshi Idi Amin 1971. Alirudi tena madarakani 1980 alipoangushwa Amin kwa msaada wa majeshi ya Tanzania 1979. Lakini alipopinduliwa mara ya pili miaka mitano baadae, akakimbilia uhamishoni nchini Zambia alikofariki 2005.
Uhusiano wa KK na Mwalimu pamoja na Jamhuri ya Umma wa China ya Mwenyekiti Mao Tse-Tung, ulifanikisha ujenzi wa njia ya reli kutoka Tanzania hadi Zambia iliojulikana kama reli ya Uhuru kutoka Dar-es-saalaam hadi Kapiri mposhi mwanzoni mwa miaka ya 1970. Ulikuwa mradi wa kwanza wa msaada wa China nchi za nje. Mshikamano mkubwa zaidi wa viongozi hao wawili.
Viongozi hao wawili alishirikiana bega kwa bega katika harakati za kupigania Kusini mwa Afrika. Wakati Tanzania ilikuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi barani Afrika na Kamati ya ukombozi ya Umoja wa nchi huru za Afrika OAU, Zambia ilivipa ofisi na hifadhi vyama vya ukombozi wa Zimbabwe, Zimbabwe African People´s Union (ZAPU) cha Joshua Nkomo na Zimbabwe African National Union (ZANU) kilichoongozwa kwanza na Ndabanigi Sithole na baadae Robert Mugabe.
Licha ya mashambulizi ya utawala wa wazungu wachache wa Ian Smith ndani ya Zambia,wakati huo Zimbabwe ikiitwa Rhodesi sini, msimamo wa Kaunda haukutetereka.
Kaunda na Nyerere wakifahamiana tokea wakati wa harakati za kupigania nchi zao kujitoa kwenye ukoloni.
Kaunda alikuwa ameshanza kujihusisha na harakati za Umajimui wa Afrika na kashiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Pan African Freedom Movement for East , Central and Southern Africa ( Jumuiya ya kupigania uhuru wa nchi za Afrika Mashariki, kati na Kusini)-PAFMECA.
Miongoni mwa wanasiasa waliokuwa katika Jumuiya hiyo ni Joshua Nkomo wa Rhodesia Kusini, Kamuzu Banda na Kanyama Chiume Nyasaland, na Abdulrahman Babu kutoka Zanzibar. Wote walijiunga na wanasaiasa wengine wa Afrika kuhudhuria mkutano ulioitishwa 1962 na Rais Kwame Nkrumah mjini Accra Ghana.
Bendera ya Uingereza ilipoteremshwa Rhodesia Kaskazini Oktoba 24, 1964 na kuzaliwa taifa jipya Zambia, Kaunda akawa Kiongozi wake wa kwanza. Aliamua kujitolea kuvisaidia vyama vya wapigania uhuru kusini mwa Afrika. Pamoja na Rais Julius Nyerere wa Tanzania walikuwa waasisi wa kundi la nchi za mstari wa mbele, lililowajumisha pia viongozi wa, Angola, Msumbiji na Botswana, zilizokuwa nguvu iliyzisukuma harakati za ukombozi Zimbabwe, Namibia na hatimaye Afrika Kusini.
Licha ya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Zambia ya utawala wa wazungu wa Ian Smith katika Zimbabwe iliojulikana wakati huo kama Rhodesia kusini, msimamo wa Dk Kaunda haukutetereka.
Dk Kenneth Kaunda na kitambaa cheupe mkononi kama ishara ya amani atakumbukwa kwa kauli yake mbiu `One Zambia , One Nation´ (Zambia moja, taifa moja) iliosaidia kudumisha umoja, amani na utulivu nchini mwake. Anajiunga na rafiki yake Julius Nyerere aliyefariki mwaka 1999, wakati Afrika ikiwa imempoteza shujaa wake wa mwisho wa kizazi cha waliopigania uhuru wa nchi zao na heshima ya bara hilo.