Macron ametaka Johnson kutimiza ahadi juu ya Brexit
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemuambia Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuwa mahusiano ya mataifa hayo mawili yataanzishwa tena iwapo atasimamia ahadi zake kuhusu mpango wa Brexit aliyosaini na Umoja wa Ulaya. Tangu Uingereza ilipojiondoa katika Umoja huo mwishoni mwa mwaka uliopita uhusiano kati yake na Umoja huo hasa Ufaransa umeyumba. Katika mkutano wa kundi la nchi tajiri duniani G7 unaofanyika Kusini Magharibi mwa Uingereza, Macron alimuambia Johnson kwamba mataifa yote mawili yana masilahi sawa lakini uhusiano wao utaimarika atakapotimiza ahadi. Boris Johnson anataka mkutano wa G7 ujadili kwa upana masuala ya kimataifa, lakini ameendelea kushikilia msimamo wake wa kuutaka Umoja wa Ulaya kurahisisha biashara kati ya mpaka wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini.

