Mamlaka ya Wapalestina jana imefuta mpango wa kupokea chanjo za Covid-19 zilizosalia na muda mchache wa matumizi kutoka Israel, baada ya shehena ya kwanza kutoka Israel kuonyesha tarehe ya mapema zaidi ya kuisha muda wa matumizi kuliko walivyokubaliana.
Waziri wa Afya wa Palestina Mai Alkaila amewaambia waandishi wa habari kuwa wamekataa dozi hizo kwasababu muda wake unamalizika mwezi Juni na katika makubaliano waliambiwa muda unakamilika Julai ama Agosti.
Israel na Mamlaka ya Wapalestina walitangaza mpango wa kubadilishana chanjo hiyo mapema Ijumaa ambapo yangeshuhudia Israel ikipeleka dozi milioni 1.4 za chanjo ya Pfizer-BioNTech kwa mamlaka ya Wapalestina, kwa makubaliano ya kupokea idadi ya sawa ya dozi kutoka mamlaka ya Wapalestina baadae mwaka huu.
Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett ilipotangaza makubaliano kati yake na Palestina ilisema kuwa chanjo hizo zinazikaribia kumalizika muda wa matumizi. Lakini waziri Alkaila amesema kilichokubaliwa sicho na hivyo wameamua kurejesha hata shehena ya kwanza ya dozi karibu elfu 90 nchini Israel.