Serikali ya Tanzania imesema kuna viashiria vya wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona kuingia nchini kutokana na nchi jirani wananchi wake kuzidi kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Juni 19, 2021 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mkurugenzi wa kinga wa Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi ametoa maagizo kadhaa likiwemo la kuwataka wananchi kuvaa barakoa.
“Wizara inawakumbusha wananchi wote kutopuuza ugonjwa wa Covid-19. Wizara imeanza kuona viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la mlipuko wa ugonjwa huu katika nchi yetu.”
“Hii ni kutokana na taarifa za ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa huu zinazofanywa na wizara na mwingiliano kati ya watu wetu na mataifa mengine,” amesema Dk Subi.
Amesema idadi ya wagonjwa wanaokutwa na vizuri vya corona barani Afrika imeongezeka ndani ya wiki tano mfululizo zikiwemo nchi jirani na Tanzania, “maambukizi yanaongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa wimbi la pili.”
Katika maelezo yake amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.