Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amelitaka kundi la mataifa 7 yenye nguvu ya kiviwanda duniani kulifadhili Shirika la Afya Ulimwenguni WHO katika mpango wake kuongezea nguvu kampeni za upimaji wa Covid-19, uchunguzi na utoaji chanjo.Akizungumza baada ya kupata fursa ya kuhutubia mkutano wa kilele wa mataifa hayo nchini Uingereza hapo jana, Ramaphosa, amesema mataifa hayo ambayo yanachangia zaidi ya nusu ya pato jumla la ulimwengu, yanapaswa kutoa kiasi cha dola bilioni 16.8 kuziba pengo lililopo kwa mwaka huu.Kwa mujibu wa WHO, takribani asilimia 90 ya mataifa ya Afrika hayatoweza kufikia lengo la kuchanja asilimia 10 ya watu wake ifikapo Septemba, katika kipindi hiki ambacho bara hilo linakabiliwa na wimbi la tatu la kusambaa kwa virusi vya corona.Kwa mujibu wa majumuisho yanayofanywa na shirika la habari la Uingereza-Reuters, Afrika ina visa milioni tano vya maambukizi ya virusi vya corona, na eneo la kusini la bara hilo ndilo lililoathiriwa zaidi.
