HADHI ya Tanzania ni mshikamano wa Kiafrika, kupigania haki na usawa, kutetea misimamo yake katika diplomasia kwa kushirikiana na majirani zake na mataifa mengine katika masuala ya ulinzi na usalama na ndiyo maana imekuwa kinara wa sera za ukombozi kupitia nafasi yake ya Uenyekiti wa Nchi za mstari wa mbele kusini mwa Afrika, ambapo ilihifadhi na kuwafadhili wapigania uhuru kusini mwa Afrika pamoja na wanasiasa mbalimbali ambao leo hii ni vingozi wa ngazi za juu katika nchi jirani zake.
Hata hivyo taswira hiyo ilikuwa tofauti katika ngwe ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano ya hayati Dkt. John Magufuli kisha kijiti cha uongozi kukabidhiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ndani ya siku 100 madarakani hajabadilisha mambo kwa upande wa masuala ya ulinzi na usalama, kushiriki utatuzi wa migogoro, kupambana na ugaidi kwa kuwasaidia jirani yake Msumbiji.
Ujasiri uliooneshwa na Tanzania ni kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kwa mataifa mawili ambayo awali yalikuwa kwenye 'vita baridi' tangu uongozi wa rais wa kwanza Julius Nyerere, yaani Israel na Morocco. Serikali ya Magufuli ilifungua ubalozi nchini Israel na kuanza ushirikiano nao licha ya taifa hilo kulaumiwa kwa ukatili na mabavu dhidi ya Mamlaka ya Palestina. Pia mwanamfalme wa Morocco Hassan V alizuru Tanzania licha ya nchi hiyo kulaumiwa kuikalia kimabavu Sahara Magharibi. Mahusiano hayo yalikuwa ni 'tangazo' la enzi mpya za Diplomasia ya Tanzania.
Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 19 mwaka 2021 kutokana na kifo cha mtangulizi wake, Dkt. John Magufuli, ambapo siku 100 za kwanza za urais katika taifa lolote duniani hutumika kufanya tathmini ya uongozi mpya, kwa upande wake ameonesha mwelekeo uleule wa 'kukalia kimya' masuala ya ushirikiano wa ulinzi na usalama kwa majirani zake.
Ikumbukwe wakati wa awamu ya nne chini ya rais mstaafu Jakaya Kikwete Tanzania ilisifika kwa ushirikiano ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali. Mathalani kupambana na waasi nchini Comoro,ushiriki katika vikosi vya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),Sudan na Lebanon kwa kuzitaja chache.
Ukimya katika mgogoro wa Msumbiji
Msumbiji ni nchi mwanachama wa SADC na inasumbuliwa na magaidi tangu Oktoba mwaka 2017, ambapo duru za ulinzi na usalama zinamtaja kiongozi wa wahalifu hao ni Abu Yusir Hassan.
Magaidi ambao wanatajwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi cha ISIS wamekuwa wakifanya hujuma dhidi ya raiana serikali ya Msumbiji katika mji wa Palma uliopo maili sita kutoka kwenye mradi mkubwa wa gesi asilia katika eneo la Afungi,Macimboa de Praia na mengine ya jimbo la Cabo Delgado.
Januari mwaka 2021 hayati Magufuli alikutana na mwenzake wa Msumbiji Felipe Nyusi ambapo taarifa zinabainisha kuwa ajenda mojawapo ilikuwa hali ya ulinzi na usalama katika mipaka ya nchi zao. Hata hivyo hapakuwa na taarifa wala matokeo ya ajenda hiyo kwani sakata la magaidi limeendelea kuchafua taswira ya Msumbiji,kutishia usalama wa majirani zake na kuonesha kana kwamba SADC imefeli katika kushughulikia usalama wa nchi wanachama.
Mamlaka za Tanzania hazijawahi kuzungumzia matatizo ya ugaidi ya jirani yake huyo na sasa siku 100 zimeyoyoma, Rais Samia hajazungumzia ingawa hivi karibuni alimtuma rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi kumwakilisha katika moja ya mikutano ya jumuiya hiyo. Hata Tanzania ilipokuwa Mwenyekiti wa SADC, hapakuwa na ajenda mahususi ya wazi mapambano dhidi ya magaidi waliopo Msumbiji.
Je ni njia ipi mwafaka kwa Samia katika ulinzi na usalama?
Duru za ulinzi na usalama kuwa Tanzania imekuwa katika mwelekeo tofauti, huku baadhi ya wataalamu kutoka vyombo vya dola wanabainisha sababu mbalimbali zikiwemo hatari kwa taifa kujihusisha na mizozo ya kigaidi,kutamalaki ukosefu wa usiri miongoni mwa washirika.
"Hilo ni suala nyeti, ifahamike miaka 1980 hadi 1988 majeshi ya Tanzania yalikuwepo nchini Msumbiji, ila baadhi yao si watuwaaminifu ni rahisi kuwaonesha maadui zenu wapi mpo na namna mnavyofanya shughuli. Rushwa huathiri mwenendo wao wa ushirikiano kwenye ulinzi n usalama na kupunguza wataalamu wake. Mipaka yetu italindwa bila kujali nje wanazungumza nini, lakini mamlaka inajua nini cha kufanya na kipi isifanye," amesema mmoja wa wataalamu hao.
Aidha, kwa namna fulani Tanzania inapaswa kuchukua hatua madhubuti kushirikiana na Msumbiji kukabiliana na janga la ugaidi, kwa sababu iwapo majirani hao mmoja akikosa utulivu sababu ya matukio hayo maana yake mwingine ataathirika kwa namna mbalimbali hivyo ni vema kutanzua mizozo ya namna hiyo mapema kabla ya haijajenga ukongwe na kuwa ngumu kumalizwa.
Kuchelewa kuchukua hatua ni kusogeza mbele nguvu za magaidi bila kujali ikiwa Rais Samia ana matazamo sawa na Magufuli au tofauti na Jakaya Kikwete na wengine.
Vilevile jeshi la pamoja EAC iwe ajenda maalumu ili kutimiza matakwa ya kimkataba na kuchochea mshikamano pale mwanachama mmoja anapokabiliwa na makundi ya waasi na kadhalika.
Wakati nchi kama DRC, Somalia zikitamani kujiunga na EAC, ni vizuri wanachama wa sasa wakaonesha kuwa wapo tayari kuziunganisha nchi zao kwenye masuala yote yaliyokubaliwa kwa maslahi ya wananchi. Kwa kuanzia ni kuzingatia suala la ushirikiano wa ulinzi na usalama, iwe sirini au hadharani kwa sababu ni wa lazima kwa minajili ya kuhami uchumi wa mataifa yenyewe.