Siku ya Wkimbizi duniani: Je ni kwanini Wakimbizi kutoka Congo hawafurahii siku hii

Wakimbizi kutoka DR Congo
Maelezo ya picha,

Wakimbizi kutoka DR Congo

Siku ya wakimbizi imesherehekewa leo kote duniani. Nchini Rwanda baadhi ya wakimbizi kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema hawana cha kusherehekea kwa madai ya ugumu wa maisha wanayoishi ukimbizini .

Kambi ya Gihembe kaskazini mwa Rwanda ndiyo kambi iliyodumu kwa muda mrefu yaani miaka 24 ikiwa inahifadhi wakimbizi zaidi ya elfu 10 kutoka DRC .Kuna baadhi walizaliwa katika kambi hiyo na wao pia kwa sasa ni wazazi.

Ingabire, 24 aliolewa yapita miaka 3 unusu na ana mtoto mmoja .Alisema aliolewa akiwa mdogo kutokana na ugumu wa maisha kambini.

''unajua mtoto wa kike anahitaji mambo mengi na hapa kambini maisha hayaruhusu wazazi kotosheleza mahitaji ya watoto, ndiyo maana niliamua kuolewa. Sasa niko nyumbani kwangu ni kama nasimamia maisha yangu''alisema Ingabire.

Baadhi ya wakimbizi hufanya vibarua nje ya kambi na kuna wachache wanaofanya biashara za rejareja ndani ya kambi.

Ingabire anasema yeye hana kazi yoyote isipokuwa ''kuamka kila asubuhi na kufanya usafi nyumbani ,kisha anatazama ikiwa kuna chakula kinachoweza kupatikana ili niweze kukitayarisha.Vinginevyo kwangu siku zote ziko sawa''

Wasikitishwa na kutojua nchi yao asilia

Wakimbizi katika kambi ya Gihembe walikimbia vita na machafuko DRC mwaka 1997 na kukimbilia nchini Rwanda .Ingabire aliambia BBC kwamba alipokuwa mtoto ndipo alifahamishwa na wazazi wake kwamba nchi yao asilia ni Congo, eneo la Masisi.

''Kuna wakati nakaa na wazazi wangu wakiwa wananipa hadithi za Congo na historia yake. Nasikitika sana ninapofikiria maisha mabaya ninayoishi hapa Rwanda na namna wazazi wangu wanavyoniambia kwamba huko Masisi walikuwa na mashamba, na ng'ombe, kweli natamani kujua nchi yangu kuwa na hamu kubwa kwamba siku moja tu nitarudia katika nchi yangu''

Kambi ya Gihembe inahifadhi wakimbizi zaidi ya elfu 10.
Maelezo ya picha,

Kambi ya Gihembe inahifadhi wakimbizi zaidi ya elfu 10.

Kambi ya Gihembe inahifadhi wakimbizi zaidi ya elfu 10. Tangu mwezi wa tatu mwaka huu shirika la mpango wa chakula duniani WFP lilipotangaza kupunguza msaada wa chakula kwa wakimbizi wote waliopo nchini Rwanda ,wengi wanalalamikia kuwa na maisha magumu.

''Ni vizuri kwamba waliweka siku kuu hii. lakini mimi siwezi kuwa na furaha na sina cha kusherehekea wakati ambapo bado napangiwa namna ya kuishi. wakati ambapo bado naishi katika nchi isiyo yangu, siwezi kusema kwamba nasherehekea''Alisema Ingabire.

Wakati wa ziara yake nchini Rwanda mwezi April mwaka huu, Kamishna mkuu wa shirika la kimataifa la wakimbizi UNHCR Filippo Grandi alisema kwamba shirika lake na mataifa ya Rwanda na DRC bado wanafanya mazungumzo ya jinsi ya kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Congo likizingatiwa pia swala la usalama mdogo katika maeneo walikotokea ya mashariki mwa DRC.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post