Taliban yasema mfumo wa Kislamu ndio njia pekee kwa amani Afghanistan
Kundi la Taliban, limesema leo kwamba limejitolea kwa mazungumzo ya amani. Lakini limesisitiza kwamba kile walichokitaja kuwa “mfumo halisi wa Kiislamu” nchini Afghanistan ndiyo njia pekee ya kumaliza vita na kuhakikisha haki zinalindwa ikiwemo za wanawake.Mazungumzo kati ya wanamgambo wa kundi hilo pamoja na serikali ya Aghanistan yamekwama kwa miezi kadhaa na machafuko yamezidi kuongezeka maeneo kadhaa nchini humo tangu mwezi Mei wakati wanajeshi wa Marekani walipoanza kuondoka.Hofu inaongezeka kwamba ikiwa kundi la Taliban litarejea madarakani, litarudisha tena aina ya sheria yao kali ya Kiislamu, ambapo wasichana wanapigwa marufuku kwenda shuleni na wanawake ambao wametuhumiwa kuhusika na uzinifu, hupigwa mawe hadi kufa viwanjani.Licha ya machafuko kuongezeka, muasisi mwenza wa kundi hilo ambaye pia ni naibu kiongozi Mullah Abdul Ghani Baradar, amesema leo kwamba kundi hilo limejitolea kwa mazungumzo ya amani.