Tanzania-Uganda: Ramani ya Afrika mashariki ingekuwa tofauti na ilivyo sasa iwapo Amin angeshinda vita vya Kagera

 

Nyerere, Obote and Jomo Kenyatta form EAC

CHANZO CHA PICHA,TANZANIAGOV

Vita kati ya Uganda na Tanzania vilizuka Oktoba mwaka wa 1978 na matokeo yake endapo yangeipa Uganda ushindi ,yangebadilisha kabisa ramani ya afrika mashariki kama ilivyo sasa .

Chanzo kikuu cha mapigano hayo kilitokana na hatua ya rais wa Uganda wa wakati huo Idi Amin kutangaza kwamba eneo la Kagera lilifaa kuwa sehemu ya Uganda.Hatua hiyo ilimlazimu rais wa Tanzanzia wakati huo hayati Julius Nyerere kutangaza vita dhidi ya Uganda na baadaye kusaidia kumuondoa Amin madarakani .

Hali zilizozingira kuzuka kwa vita hazieleweki, na sababu nyingi tofauti za tukio hilo zipo.Rais MiltonObote aliandika kwamba uamuzi wa kuvamia Kagera ulikuwa "Hatua ya kukata tamaa ya kumtoa Amin uongozini kutokana na matokeo ya kufeli kwa njama zake mwenyewe dhidi ya jeshi lake.

" Wanajeshi kadhaa wa Jeshi la Uganda walimlaumu Luteni Kanali Juma Butabika kwa kuanzisha vita pamoja na Kanali Abdu Kisuule, ambaye alimshtumu Butabika kwa kuanzisha vita kutumia tukio lililotokea mpakani ili kujenga kisingizio cha kuivamia Tanzania.

Nyerere

CHANZO CHA PICHA,GOOGLE

Kulingana na mtoto wa Amin, Jaffar Remo, uvumi wa uwezekano wa uvamizi wa Tanzania ulisababisha jeshi la Uganda kuitisha shambulio la mapema dhidi ya Tanzania.

Wanajeshi wa Tanzania baadaye walisema kwamba lengo kuu la Amin lilikuwa kuchukua sehemu kubwa ya kaskazini mwa Tanzania, pamoja na jiji la Tanga, ili kuweza kupata bahari kwa sababu za biashara.

Vita hivyo vilitanguliwa na kuzorota kwa uhusiano kati ya Uganda na Tanzania kufuatia hatua ya Amin kupindua serikali ya Rais Milton Obote na baadaye kutwaa madaraka mnamo 1971.

Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, alikuwa na uhusiano wa karibu na Obote na aliunga mkono jaribio lake la kuanzisha uasi Uganda mnamo 1972, na kusababisha mapigano ya mpaka na mwishowe kusainiwa kwa makubaliano na Amin ambayo yaliafikia kwamba viongozi wote wataondoa vikosi vyao kutoka mpakani.

Walakini, uhusiano kati ya marais hao wawili ulibaki kuwa wa wasiwasi, na Amin alianza kudai kwamba eneo la Kagera — sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania kati ya mpaka rasmi na Mto Kagera, inapaswa kuwekwa chini ya mamlaka ya Uganda. Kwa miaka iliyofuata, utawala wa Amin ulidhoofishwa na vurugu, shida za kiuchumi, na kutoridhika katika Jeshi la Uganda.

Mnamo Oktoba 1978 vikosi vya Uganda vilianza kuingia nchini Tanzania. Baadaye mwezi huo Jeshi la Uganda lilianzisha uvamizi, likipora mali na kuua raia. Vyombo rasmi vya habari vya Uganda vilitangaza kutwaliwa kwa eneo la Kagera.

Uchokozi wa Amin ulianzia hivi

Ripoti zinaonesha kuwa katika wiki za mwanzo wa mwezi Septemba 1978, kikosi cha jeshi la Tanzania kilichokuwa kinalinda mpaka lilikuwa kinashuhudia kuongezeka kwa shughuli za jeshi la Uganda ikiwemo ongezeko lisilo la kawaida la magari na wanajeshi karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Lakini kwa kuwa yote hayo yalikuwa yakifanyika ndani ya Uganda ripoti hizo awali hazikuushtua uongozi wa jeshi la Tanzania. Hata hivyo, kufikia katikakati ya Septemba, ndege za kijasusi za Uganda zikaanza kufanya doria katika anga la Tanzania kwenye mkoa wa Kagera.

Idi Amin

CHANZO CHA PICHA,HULTON ARCHIVE/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Idi Amin

Mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, kamanda wa kikosi chajeshi la Tanzania kilichokuwa kinalinda mpaka huo Luteni Kanali Morrison Singano akawa anatuma ripoti za ilani kwenda makao makuu ya jeshi kuwa kuna uwezekano wa vikosi vya Uganda kuvamia ardhi ya Tanzania. Lt. Kanali Singano aliomba kungezewa nguvu kikosi chake, lakini hilo halikutokea mpaka baada ya uvamizi kufanyika.

Mchana wa tarehe 9 Oktoba, wanajeshi wa Uganda waliingia Tanzania kwa mara ya kwanza kwa kutumia kikosi kidogo cha magari na kuchoma nyumba mbili katika kijiji cha Kakunyu.

Tanzania ilijibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora ambayo yaliharibu gari moja la Uganda na kuua wanajeshi wawili. Redio Uganda jioni ya siku hiyo iliripoti kwamba Tanzania ilijjaribu kuvamia Uganda na jeshi la nchi hiyo lilizuia uvamizi huo kutokea. Huo ulikuwa ni mwanzo rasmi wa mapambano ambao hakuna aliyedhani kwa wakati huo kuwa yangelipuka na kuwa mojja ya vita kubwa na muhimu katika historia ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujjumla.

Siku iliyofuata ndege vita za Uganda aina ya MiG zilitupa mabomu kwenye misitu ya Tanzania. Makabiliano madogo madogo yaliendelea katika eneo hilo la mpaka, Viongozi wa Tanzania walihisi kuwa Amin alikuwa akifanya chokochoko tu.

Hata hivyo, hali iliendelea kuzorota na kufikia Oktoba 18 ndege za kivita za Uganda zikashambulia makao makuu ya mkoa wa Kagera, mjji wa Bukoba. Licha ya kwamba mashambulio hayo yalikuwa na athari ndogo, lakini ilitosha kupandisha hofu wananchi ambao baadhi yao waliamua kuondoka kabisa eneo hilo na familia zao ili kunusuru maisha yao.

Mapambano ya mpakani yaliendelea kwa siku kadhaa huku ndege za Amin zikishambulia tena mjji wa Bukoba Octoba 27, huku bomu moja likianguka karibu na hospitali. Hata hivyo siku hiyo hiyo kikosi kidogo cha makombora ya kutungua ndege kutoka jeshi la Tanzania kilifika Bukoba, na siku iliyofuata kilifanikiwa kuidungua ndege moja ya Uganda.

Mnamo asubuhi ya Oktoba 30 takriban wanajeshi 3,000 wa Uganda walivamia Tanzania kwa kuingia kupitia maeneo manne ya mpaka;njia nne kupitia Kukunga, Masanya, Mutukula, na Minziro. Waliongozwa na Mkuu wa Jeshi la Uganda Yusuf Gowon na wakiwa na vifaru na magari ya APC, walikumbana tu upinzani mdogo tu kutoka kwa mgambo wa Tanzania.

Licha ya upinzani mdogo kutoka kwa vikosi vya Tanzania, wanajeshi wa Uganda walisonga mbele kwa tahadhari. Walilishika polepole eneo la kaskazini la bonde la mto Kagera, wakiwafyatulia risasi askari na raia, kabla ya kufika Mto Kagera na Daraja la Kyaka wakati wa jioni. Japo ineliwezekana kwa vikosi vya Uganda kusonga mbele mpaka Bukoba kutokana na upinzani dhaifu uliokuwepo wa vikosi vya Tanzania, vikosi hivyo viliishia katika daraja hilo.

Mnamo tarehe 1 Novemba Redio Uganda ilitangaza kile ilichokiita "ukombozi" wa Kagera na kutangaza kuwa sasa Mto Kagera uliashiria mpaka mpya kati ya Uganda na Tanzania.

Amin alitembelea eneo hilo na kupiga picha na vifaa vya vita vya Tanzania vilivyoachwa. Makamanda wa Uganda walihofu kwamba Daraja la Kyaka lingeweza kutumika katika kurahisisha mashamulizi ya Tanzania endapo ingeamua kutuma vikosi vya kulikomboa eneo hilo, kwa hivyo mnamo Novemba 3 walitumia mabomu kulisambaratisha.

Jeshi la Uganda baada ya hapo likaendesha operesheni ya kupora mali za watu, kuua maelfu ya raia wasio na hatia na pamojja na kuteka na kubaka mamia ya wanawake katika eneo hilo. Maelfu ya wakaazi walikimbia nyumba zao na kwenda kujificha msituni ama kuvuka mto na kuingia eneo la kusini la bonde la mto Kagera ambalo majeshi ya Amini hayakufika.

Wakati Amini na makamanda wake wakisherehekea ushindi, Tanzania ilijipanga napunde tu ikaanzisha mapambano ya kulikomboa eneo lake.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post