'Gold Digger' huyu ni mtu ambaye anaendeleza uhusiano na mtu mahususi kuchukua pesa na utajiri wake.
Huwa hana hisia za kweli au kumpenda mtu kwa kumaanisha na mwenza wake badala yake lengo lake katika mahusiano huwa ni kuchukua utajiri wa mwenzake.
Wakati yeyote kati yao katika uhusiano anaweza kuwa anawinda tu pesa za mwenzake, mara nyingi kuna dhana kwamba kama mtu ameoa au kuolewa na mwenza wake mwenye umri mkubwa sana kumpita, yeye ndiye aliyefuata pochi.
Na mbinu inayotumika sana kumchuna mwenza wako ni kuomba kutalakiana baada ya kuishi naye kwa muda, kusubiri aage dunia ili kurithi mali kwa njia halali kisheria ama hata kuendelea kuwa kwenye uhusiano huwa lakini atahakikisha amefanya kila hila ili kutimiza lengo lake.
Dalili za kukuonesha kuwa mwenzako amefata pesa
Aina hii ya watu, kama ilivyoelezwa hapo juu, wanaweza kutumia mbinu mbalimbali kutimiza malengo yao lakini kuna dalili fulani utakapoziona, zinaweza kuashiria kwamba yupo kujinufaisha kihela.
Huwa anapenda tu zawadi za bei ghali
Wakati unaweza kufikiria pengine zawadi nzuri kwa mpenzi wako inaweza kuwa maua au kumtungia shairi, huwa kwake hazina maana na ukimfuatilia kwa makini wakati unampa unaweza ukakutana na makunyanzi usoni ishara kuwa hajaifurahia au hata akakuuliza moja kwa moja, mpenzi, kati ya zawadi zote hii ndio umeona uniletee?
Yeye ni mtu anapendelea zawadi ambazo zina thamani kubwa ya pesa mfano magari, nyumba na kadhalika.
Wanashauku isiyo ya kawaida kutaka kujua hali yako ya kifedha
Ni kawaida sana kwa watu walio kwenye mahusiano ya uhakika au ndoa kutaka kujua hali ya kifedha ya mwenza wako.
Hata hivyo, ikiwa mtu ataanza kukuhoji unapata pesa ngapi kwa mwezi na kile ulicho nacho benki siku ya kwanza au ya pili ya kukutana, hiyo inaweza kuwa ishara tosha kwamba umekutana na mpenda pochi wala hana mapenzi kwako.
Hakuna siku hata moja atalipia matumizi yoyote
Kuwa na uwezo wa kulipia bili ya angalau kitu kimoja hakuna uhusiano wowote na kuwa tajiri.
Ni kawaida kutaka kutumia pesa zako kwa wale ambao unawapenda lakini pia kuwa na ule moyo wa kuonesha kwamba mwenzangu amenunua hiki wacha na mimi ni nunue hiki inapendeza zaidi.
Ikiwa yeye ndio mwenye kutoa tu, kununua kila kitu hata vile ambavyo anajua una uwezo wa kununua, anaweza akaanza kujiuliza, ikiwa ni hivi wakati tunachumbiana je tukioana itakuwaje?
Na ikawa ndio njia rahisi ya kumkamata aliye kwenye mahusiano kwasababu ya pesa.
Wanahadaa wengine kwa mapenzi
Kwasababu wao wapo kwa lengo la kupata pesa, wanatumia uzuri wao, maumbo yao na hila nyingine za aina hiyo kupata wanachotaka.
Wakati unafikiria kujiendeleza kwa mengine, wao hawashughuliki na suala la kuwa unataka kujikomboa zaidi kimaisha badala yake, wanafuatilia kwa karibu namna wanavyoweza kuwa wa kuvutia zaidi, warembo kwa kujinunulia vipodozi vya ghali, nguo za kifahari, mikoba ya mikononi inayotamba kwenye fasheni na kadhalika.
Wanathamini sana hadhi
'Gold diggers' wanataka kutambulika kama matajiri kwasababu lengo lao la mwisho ni kupata pesa au angalau kuonekana kwamba wao ni wa hadhi ya juu katika jamii.
Katika fikra zao, wanaamini kwamba pesa ndio kila kitu maishani na ndizo zinawawezesha kupata umaarufu au kuwa na nguvu katika jamii.
Pia wanaweza kuwachukia wale wanaoishi maisha ya chini na kuwadharau.
Iwapo utaona dalili kama hizi, pengine unaweza kuwa na sababu ya kutathmini tena uhusiano wako wa kimapenzi.
Siku zote hawana pesa
Kuna wale ambao siku za kwanza kwanza za mahusiano wanapenda kujaribu maji wajue hapa kunaingilika au nisonge mbele.
Wana matatizo kila siku, leo mpenzi gari imeharibika njiani, nisaidie na pesa nibadilishe tairi, au wanahitaji pesa kadhaa kulirekebisha.
Kuwa makini kwasababu mara nyingi wanajaribu kama wanaweza kununuliwa kile wanachotaka na kutathmini hapa pesa zipo au vipi hasa ikiwa ni mahusiano mapya na hajafanywa utafiti wake wa kina.
Mtu akiwa anajukumu sio kila wakati atakuwa anaomba kufanyiwa hiki na kile kwasababu ni ishara ya kutowajibika au kutafuta kupata pesa kwa mwenzie.
Na hata kama ni kuomba, unaweza ukauliza ikiwa anacho akukopeshe kuonyesha utu uzima.
Dalili zinaweza kuwa nyingi mno kiasi cha kutoweza kuzitaja zote ,moja baada ya nyingine.
Ukweli ni kwamba suala la mapenzi ni la mtu binafsi hakuna anayeweza kulizuia ila hata kama uko katika hali gani, unatakiwa kuwa makini hasa pale unapokuwa unatafuta kuwa katika mahusiano ya kudumu usije ukajuta baadaye.