Zambia yatangaza siku 21 kuomboleza kifo cha Kaunda
Serikali ya Zambia imetangaza kipindi cha siku 21 za msiba wa kitaifa kuomboleza kifo cha rais wake wa kwanza Kenneth Kaunda. Kaunda aliaga dunia jana jioni katika hospitali ya jeshi mjini Lusaka akiwa na umri wa miaka 97. Kupitia mtandao wa Facebook rais wa sasa wa Zambia Edgar Lungu amemsifu hayati Kaunda akimtaja kuwa shujaa wa kweli wa kiafrika. Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson pia amepeleka salamu za rambirambi kwa taifa la Zambia akisema kupitia ujumbe wa Twitter kuwa amesikitishwa na kifo cha Kaunda. Kaunda alipigania ukombozi wa nchi yake kutoka ukoloni wa Waingereza hadi uhuru ulipopatikana mwaka 1964 na kuwa rais wa kwanza wa Zambia huru. Wakati wa utawala wake wa miaka 27 alisifika kwa kupendelea njia za amani kutatua mizozo na kusaidia harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika.
