Rais Xi amekuwa mstari wa mbele kuiweka China katika ramani ya dunia
Mapema miaka ya 1960 takriban nchi 10 za Kiafrika zilianzisha uhusiano wa kibaozi na Jamhuri ya Umma wa China na nyingi zilikuwa ni zile zilizofuata siasa za mrengo wa kushoto, zikiwemo Algeria, Misri na Guinea.
Ulikuwa ni ushindi kwa China hasa kwa mtazamo wa mvutano wake wa kifalsafa na Urusi ambayo iliisaidia China wakati wa vita vyake vya ukombozi vilivyopelekea hatimaye kuundwa Jamhuri ya Watu wa China, ikiongozwa na Chama cha Kikoministi chini ya Mwenyekiti Mao Tse Tung.
Mvutano wa madola hayo mawili makubwa katika kambi ya Wakoministi uliwagawa pia wafuasi wao. Pamoja na hayo China nayo ilijiunga na mkondo wa kuvisaidia vyama vya ukombozi barani Afrika kwa hali na mali, ukiwemo msaada wa silaha na mafunzo ya kijeshi.
Mwanzo wa China kulijongelea bara la Afrika
Ziara ya Waziri mkuu wa China Chou En-Lai katika mataifa 10 ya Afrika kati ya Desemba 1963 na Januari 1964, iligeuka ufunguo wa kuanza kwa ushirikiano wa kibiashara na msaada wa China barani Afrika. Lakini alama kubwa ya ushirikiano huo ilikuwa June 1965, wakati Zhou Enlai alipofanya ziara nchini Tanzania. Ilikuwa mwaka mmoja baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ziara hiyo ilitokana kwa sehemu moja au nyengine na uhusiano wa China na mwanasiasa maarufu wa Zanzibar Abdulrahman Mohamed Babu.
Babu mfuasi wa nadharia ya Marx na Lenin na aliyevutiwa na China ya Kikoministi ya Mwenyekiti Mao Tse Tung, alikuwa rafiki wa karibu wa Chou En-Lai na wakati wa harakati za kisiasa Zanzibar akipata msaada kutoka China. Ziara ya Waziri mkuu wa China ilifanyika miezi minne baada ya Rais Julius Nyerere kuizuru China akiwa na ujumbe mkubwa wa serikali yake uliowakilishwa na wanasaiasa wa pande mbili za muungano.
Ziara ya Rais Nyerere mjini Beijing 1965 ndio iliobadili mkondo wa muelekeo wake kisiasa. Ilitajwa na Wachina kuwa iliokuwa na umuhimu mkubwa na ya kihistoria. Nchi hizo mbili zikasaini mkataba wa urafiki. Miaka miwili baadae Nyerere akatangaza Azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa. Tanzania ikawa ni nchi ya Kisoshalisti. Ulikuwa mwanzo wa China kujitanua kwa nafasi katika bara hilo, kwa kuwa na mshirika walioaminiana. Wakati Chou En-Lai alipoitembelea Tanzania, moja wapo ya masuala muhimu katika mazungumzo yake na Nyerere lilikuwa lile la ujenzi wa reli kati ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Umuhimu wa Tazara kwa uchumi wa Zambia
Mradi huo ulikuwa na lengo la kuipunguzia Zambia isiyo na bahari kuweza kusafirisha bidhaa yake ya shaba na kuipunguzia mzigo wa matatizo ya kiuchumi na hasa kutokana na kujitolea kwake katika kusaidia harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.Tanzania na Zambia zilikuwa zimeomba msaada kutoka nchi za magharibi bila ya mafanikio. Chou En-Lai alimwambia Nyerere "ikiwa nchi za magharibi hazitaki, sisi tutaijenga."
Reli TAZARA iliojengwa 1970-1975 na kujulikana pia kama reli ya uhuru, ilijengwa na wafanyakazi karibu 50,000 Wakichina. Ukigharimu zaidi ya dola 400 milioni za Kimarekani, ulikuwa mradi mkubwa kabisa wa mkopo usio na riba kuwahi kutolewa na China nchi za nje.
"Afrika inataka kuwa bora , Afrika inataka kumaliza ukoloni" yalisema mwanadiplomasia maarufu wa Kimataifa Dr Salim Ahmed Salim aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini China, na mtu aliyeongoza kampeni na hasa miongoni mwa nchi za Afrika na Ulimwengu wa tatu 1971, ili China ikubaliwa uwanachama katika Umoja wa Mataifa.
Katika kuutukuza uhusiano wake na Tanzania na mchango wa mwanadiplomasia huyo, China ilimtunukia Dr Salim, Waziri mkuu wa zamani, Medali ya juu ya Urafiki na ya kwanza kutunukiwa Mwafrika. Katika kipindi hicho chote Tanzania ilibakia nchi yenye uhusiano mahsusi na China katika bara la Afrika.
Nini Kilianza kuibadili sera ya China kuelekea Afrika
Kifo cha Mao Tse Tung Septemba 1979, kiliibadili sera ya uchumi ya China. Mabadiliko hayo yalianzishwa na mrithi wake Deng Xiaoping, akianza na sekta ya kilimo iliorudi nyuma mno wakati wa utawala wa Mao. Deng aliamini mabadiliko ya kiuchumi yanahitaji kupewa kipaumbele kuliko yale ya kisiasa.
Reli ya Tazara ilijengwa na Wachina miaka ya 1970
Mueleko wake ulisaidia kuipa China ukuaji uchumi wa haraka, kupanda kwa hali ya kimaisha na pia kufungua milango panapohusika na uhusiano wa kiuchumi na mataifa mengine duniani. Deng aliyaita mageuzi hayo kuwa mapinduzi ya pili ya China.
Mageuzi ya kiuchumi ya China yalikuwa pia na athari katika uhusiano wa kisiasa na nchi za Kiafrika. Zile nchi kama Tanzania zilizoiona China kuwa rafiki aliyesaidia harakati za ukombozi, ziliishuhudia taratibu mtazamo mpya katika uhusiano wao.
Kuporomoka kwa nchi za Kikoministi Ulaya mashariki, lilikuwa tukio jengine lililobadili siasa za dunia na kumalizika kwa kipindi cha miongo kadhaa ya mivutano na vita baridi kati ya mashariki na magharibi.Nchi kadhaa za kiafrika zilizoelemea siasa za mrengo wa kushoto, zilijikuta zikibadili mkondo kujiepusha na hali mbaya za kiuchumi ilizoziandama. Licha ya kuwa Tanzania kuwa haikutangaza rasmi linaachana na sera ya Ujamaa, lakini kivitendo nayo iliufunika ukurasa huo na kukumbatia sera za kipebari, licha ya kuzuka majina mapya kama uchumi huria au utandawazi.
China na rasilimali za Afrika
Kwa upande China ambayo sasa ni dola kubwa kiuchumi ikichukua nafasi iliokuwa ikijivunia Japan imejiunga na mataifa mengine makubwa kiuchumi kuwa muwekezaji mkubwa barani Afrika. Mkono mtupu haurambwi, ule urafiki wa miaka ya nyuma sio uliopo sasa, kipaumbele kwa China ni masilahi yake ya kiuchumi.
Manun´guniko hata hivyo yanaongezeka kwamba China pia inashiriki katika kinyanganyiro cha uporaji wa rasilimali barani Afrika kwa kisingizio cha uwekezaji. Kumekuweko na matukio kadhaa yanayotajwa kuwa ya unyanyasaji unaofanywa na Wachina dhidi ya wafanyakazi wenyeji katika nchi kadhaa za Afrika.
Miaka 100 ya Chama cha Kikoministi na uhuru wa kisiasa
Chama cha Kikoministi kimetimiza miaka 100 tangu kilipoundwa, kikiwa kimepitia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi. Lakini kwa upande wa mabadiliko ya kuwapatia uhuru wa kisiasa wananchi wake bado pengo ni kubwa.
Wachina walijaribu kudai demokrasia walipomiminika katika uwanja wa Tiananmen mjini Beijing 1989, upinzaji unaojulikana kama tukio la Juni 4 lililokandamizwa vibaya kwa vifaru vya kijeshi. Maelfu ya wapigania demokrasi walitiwa nguvuni. Demokrasi na kuheshimiwa kwa haki za binadamu bado vinabakia kuwa ndoto.
Wanaharakati hao huenda walishawishiwa na mabadiliko yalioanzishwa nchini Urusi na Mikhail Gorbachov kwa kuleta kile alichokiita Perestroika na Glasnot (Mabadiliko na Uwazi), hatua iliosaidia kuuangusha utawala wa kikoministi na kusambaratika hatimaye kwa Muungano wa Jamhuri za Kisovieti na Jamhuri 15 zulizounda muungano huo kila moja kujitoa na kuwa huru.
Wakati Chama tawala cha kikoministi nchini China kinatimiza karne moja, swali wanalojiuliza wengi wa wachina na walimwengu kwa jumla baada ya mafanikio makubwa ya kisiasa ya dola hilo la watu takriban bilioni moja na 400 milioni, lini viongozi wake wataamua kufungua milango ya mabadiliko ya kisiasa na kuwepo demokrasia na kuheshimiwa haki za binadamu nchini humo.
2018 Rais Xi Jinping, alichukua hatua kujiimarisha zaidi madarakani, alipopendekeza na kufanikiwa, kuondoa kipengele cha ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja kwa madaraka ya Urais. Ni Ishara kuwa amedhamiria kubaki madarakani muda mrefu.