Bandari ya Bagamoyo:Je, kurejeshwa kwa mazungumzo ya mradi wa Bagamoyo nchini Tanzania kuna maana gani?

 

Bandari ya Bagamoyo inatarajiwa kushughulikia mara 25 ya idadi ya makasha kama bandari ya Dar es Salam

CHANZO CHA PICHA,AFP

Maelezo ya picha,

Bandari ya Bagamoyo inatarajiwa kushughulikia mara 25 ya idadi ya makasha kama bandari ya Dar es Salam

Ajenda ya kuimarisha biashara, kufungua milango ya fursa za uchumi na kusajili miradi mipya yenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi ni sababu ambayo imetajwa kuwa muongozo wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Na katika kuzingatia hilo, mwishoni mwa wiki Rais Samia alikaribisha majadiliano mapya ya uwekezaji wa kiuchumi wa mradi wa Bagamoyo, ambao unalenga kujenga bandari kubwa zaidi katika ukanda wa Afrika mashariki.

Awali mradi huo ulisitishwa na mtangulizi wake kwa madai kuwa hauna tija kwa taifa lakini sasa Rais Samia ametaka mazungungumzo kufanyika kurejesha mradi huo.

Mwishoni mwa wiki, Rais Samia akiwa katika mkutano wa Baraza la Biashara nchini humo (TNBC) jijini Dar es salaam, alieleza kuwa serikali yake inaendeleza mpango wa utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa makaa ya Mawe huko Liganga na Nchuchuma, na iko tayari kufanya mazungumzo na wawekezaji juu ya Mradi wa Bagamoyo.

Hata hivyo hatua hiyo imepelekea kwa duru za kisiasa nchini humo kuona kuwa nia njema ya Rais Samia inaweza kuharibika ikiwa kuna changamoto ya namna ya kuingia katika mkataba, umiliki na uendeshaji katika kutazama namna nchi itakavyolipa deni husika bila kulenga maslahi binafsi ambayo yanaweza umiza nchi.

Ikumbukwe hoja hizo zimewahi kulalamikiwa na na mtangulizi wake pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari ya Dar es salaam, Deusdedit Kakonko na hivyo kusababisha kusitishwa mpango huo mwaka 2019.

Wakati mradi huo ulipositishwa ulikosolewa vikali na kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alidai ulikuwa uamuzi uliojaa dosari nyingi na kuharibu ushirikiano wa ajenda ya kuinua uchumi na sera za viwanda pamoja diplomasia kati ya taifa hilo na washirika wake China na Oman, kwani matamshi mabaya yaliyotolewa hadharani kuhusu huo kuwa 'mradi wa kikoloni' hayakuwa na afya kwa wawekezaji na uchumi wa nchi zao.

Zitto alisema hakukuwa na sababu mradi huo kupachikwa majina mabaya na kusababisha baadhi ya wawekezaji maeneo mengine kuikimbia nchi hiyo, badala kufanya nao mazungumzo.

Wimbi la sasa la kukaribisha mradi huo lilianzia bungeni baada ya Spika Job Ndugai kusifu mpango huo na kueleza kuwa 'wakati mwingine viongozi wakuu wa nchi hushauriwa vibaya' kwa sababu mradi wa Bagamoyo utaingiza meli zenye ukubwa wa mita 300.

Je ni yapi madhumuni ya mradi wa Bagamoyo?

Mosi, mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali ya Tanzania kuanzisha maeneo 14 ya ukanda maalumu wa kiuchumi ulioanzishwa mwaka 2006.

Pili, ni ubia kati ya Tanzania, China na Oman unaohusisha vijiji vya mji wa Bagamoyo vya Kondo, Zinga, Pande, Mlingotini na Kiromo. Takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2030 vijiji hivyo vitakuwa na wakazi 75,000.

Madhumuni ya mradi huo ni;

•Ujenzi wa kituo cha ukanda cha biashara na uwekezaji.

•Ujenzi wa viwanda vya bidhaa mbalimbali.

•Ujenzi wa mji wa kisasa wa makazi.

•Ujenzi wa bandari na kitovu cha usafirishaji wa mizigo.

•Ujenzi wa barabara za ndani za kuunganisha maeneo yote ya mradi kuwezesha usafirishaji wa mizigo na huduma nyingine.

•Kuimarisha diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa washirika Tanzania,China na Oman.

•Ujenzi na uanzishwaji wa taasisi nyingine

Je, ni zipi changamoto na faida kwa majirani zake?

Kwanza ni ushindani wa huduma za bandari ndilo eneo linalotakiwa kuangaliwa zaidi hususani Lamu na Mombasa, zote za Kenya. Bandari ya Bagamoyo inakusudiwa kuwa na uwezo wa kupitisha kontena milioni 20 kwa mwaka pamoja na kuwa njia kuu ya usafirishaji wa mizigo inayotoka na kuingia kwenda nchi mbalimbali.

Uganda itakuwa na fursa ya kutumia bandari ya Bagamoyo, Lamu au Mombasa jambo ambalo litaibua ushindani wa utoaji wa huduma miongoni mwa nchi zenye bandari hizo. Hii ni changamoto kwa nchi zote wenyeji Tanzania na Kenya, huku zikihusisha pande zingine yaani wateja wao.

Ramani ya bandari zilizopo katika pwani ya Kenya na Tanzania
Maelezo ya picha,

Ramani ya bandari zilizopo katika pwani ya Kenya na Tanzania

Kwa mfano nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo rais wake Felix Tshekedi alibainisha nia ya nchi yake kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa na maana kubwa ya kunufaika na fursa za kiuchumi kuanzia soko la pamoja,ushuru,ulinzi na usalama pawe na bandari hizo.

DRC ndilo taifa linalotajwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es salaam, kwahiyo inapokuja bandari ya Bagamoyo pia inakuwa chanzo kingine cha uingizaji na usafirishaji wa mizigo yao na hivyo kuwa na uwanja mpana wa kuchagua kati ya bandari hizo mbili kwa Tanzania. Kwahiyo bandari ya Lamu na Mombasa zinakuja kupata ushindani mkali zaidi ya ule wa Dar es salaam.

Aidha, kwa kukuwa Tanzania ipo katika mkakati wa ujenzi wa mradi wa Reli ya kisasa (SGR), ni dhahiri itaungananishwa na reli ya TAZARA, hivyo kuifanya Bandari ya Bagamoyo kuwa kitovu kikubwa cha kibiashara, ambacho kitazinufaisha pia nchi za Malawi na Zambia.

Pili, kuvutia fursa kwa sekta binafsi. Kupitia sekta binafsi zikiwemo za fedha, elimu, sayansi na teknolojia ya kisasa,utalii na mabwawa, ambapo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakwenda kunufaika nao. Ifahamike Bagamoyo ni mji wa kitalii, mradi huo unasisimua zaidi shughuli hizo, kwahiyo wananchi kutoka Kenya,Uganda,Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na pengine DRC watanufaika na fursa mbalimbali katika mradi huo.

Tatu, uzalishaji wa ajira ni eneo jingine ambalo litawanufaisha wanajumuiya ya Afrika mashariki na washirika wa kibiashara wa mradi na ukanda. Takribani viwanda 690 vinatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 20,000. Pia utekelezaji wa awamu ya pili na tatu ulitarajiwa kujengwa viwanda 3,258 ambavyo vitaleta ajira mpya. Kwa muktadha huo ujenzi wa viwanda utahuisha sera hiyo ambayo imekuwa ikipiganiwa na serikali ya awamu ya tano, na sasa Rais Samia anaendeleza mkakati wa huo na atafanya vizuri zaidi ikiwa mradi huo utafika makubaliano na wawekezaji.

Nne, Biashara na Masoko ni eneo litakalonufaisha nchi wanachama wa SADC na EAC kwa sababu Tanzania imesaini mikataba ya maeneo hayo pamoja na ule wa Cotonou,AGOA. Vilevile tanzania inatarajiwa kupanua soko la bidhaa zake katika nchi za Umoja wa Ulaya ku[pitia mpango wa EPA, ACP (EU-ACP) pamoja na Marekani.

Tano, Biashara ya anga. Kulingana na mpango wa mradi huo ujenzi wa kiwanja cha kimataifa cha ndege ni sehemu ya kuinua na kurahisisha usafiri kati ya Bagamoyo na mataifa ya kigeni. Hivyo basi, inatarajiwa mashirika ya ndege kutoka nchi jirani kama vile Uganda Airlines,RwandAir na Kenya Airways yatanufaika na mradi huo.

Je Rais Samia atakiwa kufanya nini kwa sasa?

Kwa kipindi cha miaka mitano na siku 114 utawala wa JPM ulikorofishana na wafanyabiashara wakubwa,kampuni,wawekezaji na mataifa ambayo yaliamua kusitisha misaada kwa Tanzania na baadhi kuhamisha shughuli zao kupeleka jijini Nairobi nchini Kenya kuwa makao yao kutokana na uhusiano hafifu.

Ili sera ya viwanda itamalaki ni muhimu kuwavutia wawekezaji wa namna hii lakini kwa masharti yenye manufaa kwa Tanzania. Bahati mbaya hayati Magufuli alisahau sera ya viwanda inawataka viongozi wa serikali kuwavutia wawekezaji matokeo yake migogoro na kampuni za kimataifa ikachukua mkondo badala ya kukaribisha meza ya majadiliano.

Hivyo ni muhimu Rais Samia anapaswa kujipanga vema kwenye meza ya majadiliano kwa kutengeneza timu ya wataalamu wa mikataba,sheria na kadhalika ili kuzishinda changamoto zinazojitokeza.

Majadiliano mapya yanakabiliwa na ushindani wa kisiasa wa pande mbili; kati ya nchi za Asia ambazo zimeweka mpango mezani na zile za Ulaya na Amerika ambazo hazijapata mradi huo. Kwa msingi huo kuhimili wimbi la ushawishi,ushindani wa kibiashara na kuwaweka sawa wawekezaji ili kuanza rasmi mradi huo, ni jaribio ambalo linasubiriwa kuonekana.

Rais Samia Suluhu Hassan

CHANZO CHA PICHA,SAMIA SULUHU HASSAN

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Soikoine na mchambuzi wa siasa na utawala bora amemwambia mwandishi wa makala haya, "Taarifa za ndani za kitaalamu zimesema mradi wa kiuchumi wa Bagamoyo ni muhimu na lazima uwepo kutokana na changamoto iliyopo katika bandari ya Dar es salaam ambayo kuanzia mwaka 2030 eneo la upanuzi wake litakuwa limefika ukomo, hivyo haitaweza kutanuliwa tena. Bandari za Lindi,Mtwara na Tanga hazikidhi mahitaji kwa kuwa zitaishia kupokea meli za ujazo wa kawaida tu wakati lengo ni kupata bandari inayoweza kuruhusu meli kubwa zaidi kutua katika ukanda huo."

Rais Samia na serikali yake wanatakiwa kuepuka hotuba zenye kuwabagaza wawekezaji na kuiga matumizi ya 'mradi wa kikoloni' kwani hujenga taswira mbaya ya mahusiano kati ya uongozi wa Tanzania na wawekezaji wa kigeni ambao wanapaswa kuvutiwa na uimara na uhusiano wao na nchi wanayotaka kuwekeza. Kama ambavyo aliziomba mamlaka za ukusanyaji wa kodi kutumia busara na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji ndivyo anavyotakiwa kushughulikia suala hili la Bagamoyo.

Kwamba lazima aepuke misuguano ya sheria za ndani na majukwaa ya kimataifa wakati wote ambao serikali yake itakuwa inakabiliana na wawekezaji wa kigeni. Kuepusha migogoro kama Makinikia ya kampuni ya ACACIA inayomilikiwa na Barrick Gold. Majadiliano kati ya serikali na wawekezaji wa Barrick Gold licha ya msuguano yalifika mwafaka, lakini bila shaka kumesalia makovu makubwa katika uhusiano wao.

Makovu ya namna hiyo yameachwa kwa taasisi mbalimbali kutoka nchi za takribani 10 kati ya 14 ambazo zilikuwa washirika wa maendeleo zilisitisha kutoa misaada yenye thamani ya dola milioni 472 pamoja na kunyimwa mpango wa MCC. Samia hatakiwi kurudi kwenye misuguano.

La kuzingatia ni kwamba hakuna mwekezaji wa kigeni atakayeionea huruma Tanzania au kulinda maslahi ya watu wake, kwahiyo ni suala la lazima kuwa na mikataba ambayo inaweka bayana manufaa ya nchi yake na namna ya kufikia.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post