Covid-19: Nini kimebadilika Tanzania tangu kifo cha Magufuli?

 

Kaburi lililochimbwa katika makao makuu ya Tanzania, Dodoma
Maelezo ya picha,

Serikali sasa imekiri kwamba corona ipo na ni tatizo

Rais Samia Suluhu alichukua hatamu za uongozi Tanzania takriban miezi mitatu iliyopita kutoka kwa John Magufuli, aliyefahamika sana kwa kutilia shaka mambo mengi kuhusu corona.

Rais Magufuli alifariki dunia mwezi Machi kutokana na matatizo ya moyo, na kifo chake kilitoa fursa ya kuwepo mtazamo mpya katika vita dhidi ya Covid-19.

Je, Tanzania imebadilika kwa kiasi gani tangu kuondoka kwa Magufuli?

Rais SKuna tofauti ya wazi katika msimamo kuhusu vita dhidi ya virusi vya corona chini ya Rais Samia katika baadhi ya mambo.

Amekiri kwamba virusi hivyo vipo na vinasambaa. Na amewahimiza Watanzania kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia barakoa na kutokaribiana.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Rais Samia Suluhu alichukua uongozi Machi mwaka huu

Hii ni tofauti sana na mtangulizi wake.

Juni 2020, baada ya taifa hilo kupitia wimbi la kwanza la maambukizi, Bw Magufuli alitangaza kuwa taifa hilo lilikuwa limevishinda virusi vya corona.

Alitangaza baadaye kuwa taifa hilo halikuwa na wagonjwa wa corona.

Pia, alipuuzilia mbali uvaaji wa barakoa na kutilia shaka chanjo zilizokuwa zimeanza kutumika kukabiliana na Covid-19. Serikali yake haikuonyesha mpango wowote wa kununua au kuruhusu matumizi ya chanjo za corona kutoka nje.

"Ninaamini... kwamba corona imeangamizwa na Mungu," alisema.

Alihimiza maombi, kufanya mazoezi, kujifukiza na tiba nyingine za asili.

Mwanamke akitoka kwenye chumba cha kujifukizia Dar es Salaam

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli alihimiza upigaji nyungu kama njia ya kukabiliana na corona

Kuhusu kujifukiza na matumizi ya tiba za asili, Rais Samia hajakuwa na msimamo wa wazi kama Bw Magufuli lakini amesema hana tatizo na matumizi ya njia hizo.

Amesema watu hawafai kuzuiwa kujifukiza, akisema amesoma pahala fulani kwani njia hiyo inaweza kusaidia katika awamu za kwanza za maambukizi, kabla ya virusi kuingia ndani sana mwilini.

Alisema sio haki kubeza kabisa na kuzikataa tiba za asili.

"Kama vinafanya kazi wacha watu watumie tu. Hatuwezi kubeza kabisa na kusema hapana tiba asili na tiba mbadala, hapana," aliwaambia wahariri majuzi.

"Kama tunahisi kufukiza nyungu kunakusaidia, nenda kafanye hivyo. Kama tunahisi sijui kumeza dawa gani kunakusaidia, kafanye."

Lakini anaeleza kuwa wanasayansi wanafaa kusaidia katika kuchunguza tiba asili mbalimbali zinazopendekezwa, na zinazofaa wasaidia kuzivumisha.

Shadrack Mwaibambe, kiongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania, anasema si vyema kwa serikali kuwa inazungumzia mambo ya kujifukiza "kwa sababu tumeamua kuifuata sayansi."

Bado hakuna ushahidi wowote kwamba kujifukiza kunaweza kutibu au kumkinga mtu dhidi ya Covid-19.

Rais amechukua hatua gani?

Alipochukua uongozi, Rais Samia aliunda kamati ya ushauri kuhusu Covid-19 ambayo iliwasilisha mapendekezo yake katikati mwa mwezi Mei.

Iliishauri serikali kutambua uwezo wa virusi hivyo Tanzania hadharani, kutangaza takwimu kuhusu Covid-19 kwa umma na kuziwasilisha pia kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha, iliishauri serikali kujiunga na mpango wa kiamataifa wa kutoa chanjo unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa Covax.

Picha ya ujumbe wa Rais Samia kwenye Twitter

Siku za mwanzo baada ya kuchukua uongozi, Rais Samia mwenyewe alikuwa akitokea kadharani bila barakoa.

Alivalia barakoa katika safari zake nje ya nchi Uganda na Kenya, lakini alikuwa akirejea Tanzania bila kuvalia barakoa.

Lakini siku za karibuni, amekuwa akivalia sana barakoa na kuwahimiza Watanzania kuvalia barakoa pia.

Idara za serikali pia zimekuwa zikiwahimiza raia kuvaa barakoa.

Na sasa kumetolewa mwongozo mpya kuhusu kufunguliwa kwa shule na taasisi nyingine za mafunzo, ambapo ni pamoja na kuvaliwa kwa barakoa, watu kutokaribiana, kuwepo vituo vya watu kunawa mikono na pia kuwepo kwa vitakasa mikono.

Hali nyanjani imebadilika?

Bw Mwaibambe, kiongozi wa chama cha madaktari, anasema kuwepo kwa utashi wa kisiasa kumebadilisha sana mambo kuhusu juhudi za kukabiliana na virusi vya corona.

Utashi huo umewaruhusu madaktari kufanya kazi kwa uhuru zaidi, kuwapa wagonjwa vipimo na majibu sahihi na kuwatibu bila wasiwasi kwa kuadhibiwa na serikali.

Wataalamu sasa wanachangia sera ya serikali, hatua ambayo anasema ni ya muhimu sana.

Awali, madaktari walikuwa hawawezi kumwambia mgonjwa ana corona na walitumia semi kama matatizo ya kupumua au nimonia isiyo ya kawaida katika kuuelezea ugonjwa.

Chini ya Rais Magufuli, Tanzania ilikuwa moja tu ya mataifa machache Afrika ambayo yalikuwa hayajajiunga na Covax.

Lakini taifa hilo sasa limesema lilijitokeza kujumuishwa kabla ya siku ya mwisho 15 Juni.

"Kwa hivyo tukaharakisha tukasema na sisi tumo, mengine ya kuagiza na chanjo ipi na nini yatafuata, lakini tumeharakisha kusema na sisi tumo," Rais Samia alisema.

Mapema Juni, alikuwa ameyaruhusu mashirika ya kimataifa na mabalozi kuingiza chanjo Tanzania kwa ajili ya wafanyakazi wao.

Umoja wa Afrika umesema pia kwamba taifa hilo linashiriki mpango wa pamoja wa kununua chanjo kupitia umoja huo.

Lakini ni muhimu kusema kwamba upo wakati ambapo Rais Samia ameonekana kuunga mkono wasiwasi kuhusu chanjo, akisema Tanzania itafanya uamuzi wake huru kuhusu suala hilo.

Akihutubia Baraza la Iddi katikati mwa Mei, alisema alifahamu kuwa walikuwa wametoa angalizo kuhusu suala la chanjo, na akasema serikali yake haitapokea "kila kitu tunacholetewa ama kuambiwa. La hasha!"

"Kwa hiyo, hata suala la chanjo nalo tutajiridhisha kabla ya kuamua kutumia au la."

Na takwimu kuhusu wagonjwa wa corona je?

Hakujakuwa na dalili zozote za kutolewa kwa takwimu za mara kwa mara za Covid-19 kwa umma, kama ilivyokuwa mapendekezo ya kamati iliyoundwa na rais.

Mapema janga lilipoanza mwaka jana, Tanzania ilikuwa ikichapisha takwimu hizo lakini hilo likasitishwa mwezi Mei 2020.

WHO imekuwa ikiihimiza serikali kuwasilisha takwimu hizo.

"Tunaendelea kuihimiza nchi hiyo kutoa data kwa WHO mara kwa mara kama yafanyavyo mataifa mengine wanachama," anasema Dkt Matshidiso Moeti, mkurugenzi mkuu wa WHO kanda ya Afrika.

Kiongozi wa upinzani Zitto Kabwe pia ameihimiza serikali kuweka wazi takwimu kuhusu visa vya maambukizi ya Covid-19 na vifo.

President Magufuli

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Rais John Magufuli: Tanzania iliacha kutoa takwimu za corona mwaka jana

Rais Samia mwenyewe alikuwa hajatoa takwimu zozote hadi mwezi uliopita.

Katika hafla na wahariri jijini Dar es Salaam, alitangaza takwimu za wagonjwa wa corona.

Lakini hakujakuwa na takwimu nyingine zilizotolewa kuhusu walio na virusi hivyo, waliolazwa hospitali au waliofariki.

Wizara ya Afya ya Tanzania haijajibu maswali yetu kuhusu kwa nini takwimu hazitolewi hadharani mara kwa mara.amia amesema nini kuhusu Covid?


Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post