Idadi ya vifo vya Covid-19 yapindukia 400,000 nchini India
Idadi ya vifo vinavyotokana na maradhi ya Covid-19 nchini India vimepindukia 400,000 leo na kufanya taifa hilo la Asia kuwa la tatu ulimwengu kwa idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kutokana na janga la virusi vya corona. Nusu ya vifo hivyo viliripotiwa wakati India ilipokumbwa na wimbi la pili ya virusi vya Corona kati ya mwezi Aprili na Mei ambalo lilitikisa mifumo ya afya huku maeneo ya makaburi na vituo vya kuchoma maiti vikizidiwa. Wakati huo huo, wizara ya afya ya India imetangaza vifo vingine 853 katika muda wa saa 24 zilizopita na idadi ya maambukizo 46,000 na kufanya jumlya ya visa vya Covid-19 kupindukia milioni 30 nchini humo. Ingawa India ni ya tatu kwa idadi kubwa ya vifo duniani ikiwa nyuma ya Marekani na Brazil takwimu zinaonesha ishara ya kupungua kwa kiwango cha maambukizo ya virusi vya corona licha ya kusuasua kwa kampeni yake ya kutoa chanjo kwa umma.