Israel yaishambulia kambi ya Hamas
Jeshi la Israel limesema kuwa limeishambulia kambi moja inayotumiwa na wapiganaji wa Kipalestina wa kundi la Hamas linaloongoza Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo. Taarifa iliyotolewa na jeshi imesema shambulizi hilo limefanywa kujibu urushaji wa maputo ya moto ambao umekuwa ukiendelea kutoka pwani ya Ukanda wa Gaza na kusababisha moto kwenye misitu na mashamba kusini mwa Israel. Mara kadhaa wapiganaji wa Kipalestina hurusha maputo yaliyosheheni mabomu na aina nyingine ya vifaa vya miripuko kwenye maeneo ya mipaka kwa lengo la kufanya uharibifu upande wa Israel. Shambulizi hilo la jeshi la Israel limefanywa wiki kadhaa tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya wapiganaji wa Kipalestina na Israel yaliyozuka mnamo mwezi Mei na kusababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 255 na Waisraeli 13.