Kwanza waliondoka Afghanistan, na sasa Iraq. Wakati wa ziara ya Waziri mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi katika White House Jumatatu, ilitangazwa kuwa majeshi yote ya Marekani yanayopigana vita yatakuwa yameondoka nje ya Iraq kufiia mwishoni mwa mwaka huu kama sehemu ya mkakati wa mazungumzo baina ya nchi mbili.
Hii iliibua maswali mawili muhimu: Hii italeta tofauti gani ndani ya Iraq?Na je hii itatoa fursa ya kurejea kwa kile kinachoitwa Isramic State (IS), kikundi ambacho kimekuwa tisho katika sehemu kubwa ya Mashariki ya Kati na kuwaajiri wafuasi kutoka mbali kama vile Uingereza, Trinidad na Australia?
Miaka kumi na minane baada ya uvamizi wa majeshi ulioongozwa na Marekani dhidi ya Iraq, Marekani ikiwa na majeshi 2,500 pekee katika ardhi ya Iraq, pamoja na idadi ndogo ambayo haijafichuliwa ya wanajeshi wa kikosi maalum kinachopigana na IS.
Walikuwa katika ngome tatu tu, ambazo ni sehemu ndogo ya kikosi thabiti cha wanajeshi 160,000-ambao waliiteka Iraq baada ya uvamizi, lakini bado wanashambuliwa na makombora na mashambulio ya ndege zisizokuwa na rubani yanayoshukiwa kutekelezwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.
Kazi ya jeshi la Marekani ni kutoa mafunzo na kuwasaidia wanajeshi wa usalama wa Iraq ambao bado wanakabiliana na mashambulio ya mara kwa mara ya mauaji yanayofanywa na wapiganaji wa IS.
Lakini uwepo wa jeshi la Marekani nchini humo ni suala lenye utata Wanasiasa wanaounga mkono Iran na wapiganaji wanawataka Marekani waondoke nje ya Iraq, hususan baada ya Marekani kumuua mkuu wa kikosi cha Iran -Iran's Revolutionary Guard's Quds Force, Jenerali Qasem Soleimani, na Kamanda wa ngazi ya juu wa Waislam wa madhehebu ya Shia kwenye uwanja wa ndege alipokuwa akitoka Baghdad mwezi Januari 2020.
Hata Wairaq wasioegemia upande wowote wangependa kuona nchi yao inawaondoa wanajeshi wa kigeni, kwasababu uvamini wa kigeni ni suala lenye utata.
Kuna wengi Washington wanaoafiki hili, ingawa sio kwa garama ya "kuikabidhi Iraq kwa Iran."
Marekani imekuwa ikijaribu kujiondoa katika kile ambacho Joe Biden anakiita "vita vya milele" katika Mashariki ya Kati.
Islamic State 2.0?
Mwaka 2011, wakati aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo , Barack Obama alitangaza kwamba vikosi vya Marekani vilikuwa vinaondoka nchini Iraq. Tangu wakati huo wamebaki wanajeshi wachache wa Marekani nchini Iraq.
Lakini kupungua huko kwa wanajeshi, pamoja na mchanganyiko wa siasa mbaya za Iraq na vita vinavyo shamiri kwenye eneo lote la mpaka nchini Syria, vilitoa nafasi nzuri kwa IS hatimaye kuiteka Mosul, mji wa pili kwa ukubwa, na baadaye ikadhibiti eneo lenye ukubwa wa nchi ya Ulaya.
Hili linaweza kutokea tena sasa? Je IS 2.0 iliyoundwa upya inaweza kwa mara nyingine tena kuliweka kando jeshi la Iraq lililonyimwa usaidizi wa kivita wa Marekani?
Kuna uwezekano mdogo wa kufanya hivyo, kwa sababu kadhaa.
IS walikuwa tayari kutumia kutoridhika kwa kiasi kikubwa kwa Waislam wa madhehebu ya Sunni nchini Iraq wakati ambapo kulikuwa na ushirika wa hali ya juu na Waziri mkuu Nuri Al Maliki.
Al Maliki aliiongoza nchi hiyo kati ya mwaka 2006 na 2014, katika utaratibu wa kuwanyima haki Wasuni, na kuwalazimisha wengi wao kuishia mikononi mwa IS.
Usawa uliopo sasa wa kisiasa, japo haujawa kamili, unakubalika zaidi miongoni mwa makundi ya kijamii yenye ushindani nchini Iraq. Tangu kushindwa kwa ISIS, Marekani na Uingereza pia wametumia muda wao wa kutosha na juhudi za kuifunza Iraq kukabiliana na vikosi vya uasi, na mafunzo yataendelea kuwepo, kwa uunganji mkono wa NATO.
Jambo la tatu ni kwamba uongozi wa ISIS, unaonesha kuwa wenye malengo zaidi kuhusu kuyatambua maeneo yaliyoachwa nyuma kiutawala katika Afrika na Afghanstan zaidi ya kupigana na makundi ya usalama yaliyojihami katika ardhi yao waipendayo ya Waarabu.
"Mashambulio ya wapiganaji wa IS yanaonekana kudhibitiwa na vikosi vya serikali ya Iraq," anasema Brigadia Ben Barry, afisa wa zamani wa jeshi la Uingereza ambaye sasa ni mchambuzi katika taasisi ya masomo ya mkakati.
Ingawa anaongeza kuwa "bila makubaliano ya kisiasa na Wasuni wa Iraq, mzizi wa sababu ya uasi utasalia kuwepo."
Islamic State waliweza kufanikiwa kufanya mashambulio kwa miaka mitano katika maeneo yote ya kanda hiyo ya Mashariki ya Kati, katika msimu wa kiangazi wa mwaka 2004, kwa upande mmoja kwasababu nchi za Magharibi zilikuwa zimeacha kuisaidia Iraq .
Ilizibidi nchi 80 ziungane kwa zaidi ya miaka mitano na kutumia mabilioni ya dola kuwashinda IS, hakuna anayetaka kupitia hayo tena.
Kwahiyo, licha ya kupunguzwa kwa idadi ya wanajeshi wa Marekani, nchi za Magharibi zitakuwa zikiangalia iwapo IS au kikundi kingine chochote cha jihadi kitaonekana kuitumia Iraq kama chambo cha kufanya mashambulizi ya kimataifa, hususan nchi za Magharibi.
"Kama Marekani ingegundua kuwa Islamic State nchini Iraq inajiandaa kufanya shambulio dhidi ya maslahi ya Marekani nje ya Iraq, huenda Washington ingeshambulia mara moja ," anasema Barr. Na kwa kuzingatia raslimali zilizopo karibu na mwambao wa ghuba, bila shaka Pentagon ina fedha za kufanya hivyo.
Mchezo wa muda mrefu wa Iran
Hapa picha ya muda mrefu ni kwamba mpaka umeipendelea Iran. Tangu yalipofanyika mapinduzi ya Kiislam y mwaka 1979, nchi hiyo imekuwa ikijaribu kuviondoa vikosi vya Marekani kwa majirani zake ili iweo dola lenye mamlaka makubwa katika kanda hiyo ya mashariki ya kati.
Imepata mafanikio kidogo kwa hilo katika mataifa ya Ghuba, ambayo yamekuwa yakiendelea kutokuwa na imani na Tehran na ambako imejenga kambi na kuendeleza shuguli za kijeshi katika nchi sita, ikiwa ni pamoja na makao makuu ya kikosi chenye nguvu zaidi cha wanamaji wa Marekani kinachofahamika kama Fifth Fleet kilichopo Bahrain.
Hatahivyo kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq, kulikoongozwa na majeshi ya Marekani mwaka 2003, kuliiwezesha Iran kupanua ushawishi wake zaidi na haijakosa fursa tangu wakati huo.
Imefanikiwa kuwaingiza wanamgambo wake wa kishia ndani ya mfumo wa usalama wa Iraq , na washirika wake wana sauti yenye nguvu katika bunge.
Vita vya wenyewe nchini Syria vimefungua fursa ya uwepo wa kiasi kikubwa cha jeshi la Iran pale, huku fursa inayofuata ikiwa ni katika nchi jirani ya Lebanon, ambaye ambako mshirika wa karibu wa Iran, Hezbollah wamekuwa ni kikosi chenye nguvu zaidi nchini humo.
Iran inacheza mchezo wa muda mrefu. Viongozi wake wanamatumaini kuwa kama watendelea na shinikizo, la wazi na la kuficha, hatimae italifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa mahala ambapo Marekani haitaona haja ya kuendelea kuweka nguvu zake za kijeshi.
Kwahivyo ndio maana ya mashambulio ya mara kwa mara ya roketi dhidi ya ngome za kijeshi za Marekani na uungaji mkono wa Iran wa maandamano ya kiraia ya kutoa wito wa kuondoka kwa majeshi ya Marekani. Makubaliano ambayo yanajumuisha kwisho wa harakati za mapigano ya Marekaninchini Iraq yataangaliwa na wengi Tehran kama yenye mwelekeo sahihi.