Kansela Merkel anakwenda Uingereza kwa ziara ya mwisho
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anakwenda Uingereza leo kwa ziara inayotarajiwa kuwa ya mwisho nchini humo kabla ya kuachia hatamu za uongozi mnamo mwezi Septemba. Ziara ya Kansela Merkel itaanza kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson yatakayofanyika kwenye makaazi ya mapumziko huko Buckinghamshire baadaye leo mchana. Mazungumzo kati ya Merkel na Johnson yatatuama juu ya kuimarisha zaidi mahusiano baina ya nchi hizo mbili baada ya Brexit pamoja na njia za kudhibiti janga la virusi vya corona. Katika siku za karibuni, viongozi nchini Ujerumani wamezungumzia wasiwasi wa kusambaa kwa virusi vya corona kutokana na idadi kubwa ya watazamaji wanaoruhusiwa kuingia kwenye uwanja wa Wimbley kutazama mechi za Michuano ya Kandanda Barani Ulaya. Wakati wa ziara hiyo, Bibi Merkel pia amepangiwa kukutana na Malkia Elizabeth wa II kwenye kasri la Windsor kwa mkutano ulioandaliwa leo jioni.