Wanajeshi wa Marekani na washirika wake waondoka kambi ya Bagram
Afisa mmoja wa wizara ya ulinzi ya Marekani amearifu leo kuwa wanajeshi wote wa nchi hiyo na wale kutoka vikosi vya washirika wameondoka rasmi kutoka kambi ya Bagram nchini Afghanistan, iliyokuwa kitovu cha operesheni za kijeshi za Washington kwa zaidi ya miongo miwili. Kambi hiyo iliyopo kaskazini mwa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani tangu taifa hilo lilipojiingiza kwenye vita nchini humo mwanzoni mwa miaka ya 2000. Kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni kutoka kambi ya Bagram kunaamisha vikosi vya jeshi la Afghanistan vinabeba dhima ya ulinzi wa eneo hilo dhidi ya mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban ambayo yameongezka katika miezi ya karibuni. Hatua hiyo ya Marekani ni utekelezaji wa uamuzi wa Rais Joe Biden wa kuondoa wanajeshi wote wa nchi yake kutoka Afghanistan ifikapo Septemba 11.