Mwekahazina wa umoja wa wafanyabiashara katika soko la Majengo jijini Dodoma, Beatrice Yame (kulia) akisimamia unawaji mikono kwa watu wanaoingia sokoni hapo kutafuta mahitaji, ikiwa ni sehemu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona. Picha na Habel Chidawali
Moshi. Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Jimbo Katoliki Moshi, zimetoa njia 19 kwa waumini wao za kukabiliana na maambukizi ya wimbi la tatu la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.
Hatua ya makanisa hayo, imekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka wazi kuwa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 100 wa corona na zaidi ya 70 wakitumia mashine.
Miongoni mwa njia zilizopendekezwa na makanisa hayo ni muumini yeyote anayeingia kanisani ahakikishe amevaa barakoa, kupunguza idadi ya waumini katika misa moja na kupunguza muda wa ibada.
Kuanzia juzi usiku na jana, ilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii taarifa ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi ambayo ilithibitishwa na Katibu wa kikosi kazi cha Bodi ya Afya ya jimbo hilo, Padri Fredrick Darkshen kuwa ni yao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu huyo alisema mapendekezo hayo 19 yametolewa na kamati maalumu iliyoundwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Minde na ilikutana Juni 26, 2021 na kuja na mapendekehayo.
“Hayo mapendekezo yametolewa na kamati maalumu kama nilivyokueleza na yatatumika katika makanisa na vigango wakati wa ibada za misa takatifu,” alisema Padri Darkshen na kuwataka waumini kuzingatia njia hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Askofu Fredrick Shoo alisema mapendekezo ya Jimbo Katoliki la Moshi yanafanana na yaliyotolewa na Dayosisi yake na kutumwa kwa wachungaji wake wote.
“Kanisa tuna wajibu wa kuwakinga waumini wetu na Watanzania katika hili wimbi baya la tatu la corona. Nimeona mapendekezo 19 ya wenzetu na sisi tulishawapelekea wachungaji wetu hayo hayo. Tuchukue tahadhari,” alisema.