Jaji alivyoainisha ubovu wa hukumu iliyowatia hatiani Mbowe, wenzake -7

 






Jana katika sehemu ya sita ya simulizi hii ya miaka mitatu ya kesi ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tuliona jinsi Mahakama Kuu ilivyoiweka katika mizania ya kisheria hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyowatia hatiani.

Katika mizania hiyo ya kisheria, Jaji Ilvin Mugeta alibainisha vigezo viwili vya hukumu bora na halali katika kesi za jinai.

Vigezo hivyo ni muundo wa hukumu na maudhui (ya hukumu husika), kuona kama hukumu hiyo iliyowatia hatiani ilikidhi viwango hivyo.

Katika uchambuzi wake amejiridhisha kuwa hukumu hiyo ilikidhi matakwa ya kisheria katika kigezo cha kwanza cha muundo huo. Sasa swali linalobaki ni maudhi yaliyomo.

Je, Jaji Mugeta amebaini nini katika kigezo hicho. Endelea kufuatilia.

Akizungumzia kigezo cha pili cha ubora wa hukumu hiyo, yaani maudhui, Jaji Mugeta anasema kwa mujibu wa hukumu ya Mahakama hiyo ya chini shtaka la kwanza la kula njama ya kutenda kosa limejadiliwa kuanzia ukurasa wa 92 hadi 94

Jaji Mugeta anasema ili kufikia uamuzi wake kwa shtaka hilo, Hakimu Mkazi Mkuu alirejea tafsiri ya kula njama katika kamusi ya kisheria ya Black’s Law Dictionary na akamnukuu kama alivyoandika, “nimesikiliza ushahidi wote wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika eneo hili. Mashahidi wa upande wa mashtaka wanaelekea kutaka kuthibitisha kosa la kula njama kama kosa la kwanza ambalo washtakiwa wote tisa wanashtakiwa nalo. Nimepitia pia mawasilisho ya hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka na upande wa utetezi. Nitatoa uamuzi baadaye katika mchakato wa hukumu hii.”

Kutokana na nukuu hiyo katika hukumu ya Mahakama ya chini, Jaji Mugeta anasema hakuna ushahidi wa mashahidi maalumu kuhusiana na shtaka hilo wala uchambuzi wa ushahidi unaoonekana katika hukumu hiyo.

Jaji Mugeta anasema hata uamuzi ulioahidiwa kufanywa baadaye (kuhusu shtaka hilo) haupatikani mahali popote katika hukumu hiyo ambayo mstari wa mwisho hakimu anaeleza,“upande wa mashtaka umeshindwa kabisa kesi yake kuhusu shtaka la kwanza.”

Kutokana na nukuu hiyo ya hukumu ya Mahakama ya chini, Jaji Mugeta anasema katika hitimisho hilo hakimu anajikanganya katika maelezo yake ya awali kwamba mashahidi wa upande wa mashtaka, “wanaelekea kuthibitisha shtaka la kula njama.”

Hivyo, Jaji Mugeta anasema haielezeki ni kwa nini sasa warufani (washtakiwa) waliachiwa huru katika shtala hilo.

Kuhusu shtaka la pili la mkusanyiko usio halali, Jaji Mugeta anasema limeshughulikiwa katika ukurasa wa 94 mpaka 95; na hakimu aliibua suala la kuamuriwa kuwa; kama Februari 16, 2018 Buibui walikusanyika (viwanjani) na kama mkusanyiko ulikuwa halali.

Katika suala hilo Jaji Mugeta anamnukuu hakimu kile alichokibaini kama alivyoandika kwenye hukumu, “siku hiyo Chadema, chama cha siasa kilikuwa na ratiba ya kufanya mkutano katika viwanja vya Buibui, na mkutano huo ulipaswa kuisha saa 12 jioni. Sikubaliani na hoja kwamba mkutano ulibadilika kuwa usio halali kuanzia wakati viongozi (wa Chadema) walipoanza kutoa maneno yanayopatikana kwenye hati ya mashtaka. Mkutano ulikuwa ni halali wakati wote wa kampeni.”

Kwa kuzingatia nukuu hiyo, Jaji Mugeta anasema baada ya hapo na bila kufanya rejea ya utetezi na ushahidi maalumu wa upande wa mashtaka, aliona ushahidi wa shahidi wa pili, wa tatu, wa nne na wa sita wa upande wa mashtaka, walithibitisha kwamba warufani wote waliondoka katika Viwanja vya Buibui na kufanya maandamano katika barabara za Mwananyamala na Kawawa.

Jaji Mugeta anasema hakimu alihitimisha suala hilo kuwa maandamano hayo yalitengeneza mkusanyiko usio halali huku akikataa kwa jumla wake ushahidi wa utetezi kwamba ni dhaifu, huku akimnukuu hakimu alivyohitimisha hoja hiyo kuwa, “washtakiwa wote walikana kufanya maandamano. Kesi ya utetezi katika eneo hili ulikuwa dhaifu na haukuweza kutikisa ushahidi imara uliotolewa na upande wa mashtaka.”

Kwa hitimisho hilo la hukumu ya Mahakama ya chini, Jaji Mugeta anasema hakimu alijiridhisha kuwa hapakuwa na mkusanyiko usio halali katika Viwanja vya Buibui (mahali ulikofanyika mkutano), bali kulikuwa na mkusanyiko mwingine usio halali katika barabara za Mwananyamala na Kawawa.

Jaji anasema utetezi dhaifu aliourejea hapo juu haukuwekwa wazi kuthibitisha hitimisho lake na kwamba wala hakuna sababu zilizotolewa kuhusu kama ushahidi dhaifu.

Pia, anasisitiza kuwa hitimisho kuwa warufani walitembea katika barabara za Mwananyamala na Kawawa ni kutozingatia kabisautetezi na kuaminika kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Jaji Mugeta anasema hakubaliani na hoja ya Wakili wa Serikali kuwa hitimisho hilo la hakimu hutokana na kuridhishwa na shahidi wa pili,wa tatu wa nne na wa sita wa upande wa mashtaka ambao ni mashahidi wa kuaminika.

Anasema sababu za kuwaona mashahidi hao kuwa wa kuaminika zinapaswa ziakisi katika hukumu yenyewe.

Kuhusu shtaka la tatu na la nne, yaani kufanya ghasia baada ya ilani (tangazo la polisi la kuwataka watawanyike”, Jaji Mugeta anarejea kile Mahakama ya Kisutu ilichokisema, “kama Mahakama hii itaona kuwa kulikuwa na ghasia na ghasia baada ya tangazo, basi itapaswa kuamua kama kulikuwa na kibali chochote kuwarusu washtakiwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.”

Lakini Jaji Mugeta anasema hakuna kitu zaidi kinachozungumzwa katika hukumu hiyo kuhusu ushahidi dhidi ya makosa hayo kabla ya kuwatia hatiani warufani (washtakiwa) na kwamba walitiwa hatiani kwa makosa hayo, maelezo matupu tu hayo hapo juu.

Jaji Mugeta anasema hukumu hiyo inayobishaniwa iko kimya juu ya tathmini ya ushahidi kuhusiana na shtaka la tano, sita na la saba na kwamba hakimu kwa kutokuwa makini baada ya kushughulikia shtaka la pili, la tatu na la nne, aliruka mpaka shtaka la tisa na la 10 ambayo ni mashtaka ya uchochezi dhidi ya Freeman Mbowe.

Jaji Mugeta anasema hakimu aliridhika kuwa makosa katika mashtaka hayo yalithibitishwa, lakini ushahidi kuthibitisha uchochezi hauwezi kuwa sawa na wa shtaka la nane la kuamsha chuki (dhidi ya Johne Heche).

Kuhusiana na shtala la 11, 12 na 13, Jaji Mugeta anamnukuu hakimu kuwa, “makosa kushawisho kutendeka kwa makosa kama yanavyoonekana shtaka la 11, 12 na la 13 nayo pia yamethibitishwa.”

Jaji Mugeta anasema hakuna sababu kuhusiana na hitimisho hilo linaloakisi hukumu hiyo na kwamba kwa urahisi namna hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu alithitimisha kuwa, “mwisho wa yote nimeridhika kwamba shtaka la 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12 na 13 yamethibitishwa bila kuacha mashaka yoyote kwa minajili ya washtakiwa wote.”

Kutokana na namna Mahakama hiyo ilivyofikia hitimisho hilo katika hukumu yake, Jaji Mugeta anasema hukumu hiyo inakosa sababu maalumu na za wazi kwa uamuzi kutokana na masuala yaliyoainishwa kwa kila shtaka waliloshtakiwa nalo, lakini hakuna uamuzi kabisa dhidi shtaka la tano, sita na saba.

Itaendelea

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post