Mahakama yaridhia diwani wa CCM kutenguliwa kwa uraia

 




Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imeridhia kutenguliwa kwa diwani wa kata ya Kagera-Nkanda, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kupitia CCM, Ezekiel Kabonge Shingo, baada ya kubaini dosari ya uraia wake.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na uhalali wa hatua na sababu za kutenguliwa katika nafasi hiyo.

Shingo alichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020, alifahamishwa kutenguliwa katika nafasi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Aprili 14, 2021 na kiti hicho kimetangazwa kuwa wazi kwa sababu za uraia wake.

Mkurugenzi huyo alichukua hatua hiyo kwa maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baada ya kufahamishwa kuwa hakuwa raia wa Tanzania kutokana na uchunguzi uliofanywa na Idara ya Uhamiaji kuhusiana na uhalali wa uraia wake.

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikifanya mchakato wa uchaguzi ili kujaza nafasi hiyo, Shingo aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba kibali cha kufungua maombi ya kupinga mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo.

Aprili 28, 2021, mahakama hiyo iliridhia maombi yake ya kibali cha kufungua maombi kupinga mchakato huo, huku pia ikitoa amri ya zuio la muda dhidi ya NEC kuendelea na mchakato huo kusubiri uamuzi wa maombi yake ya kupingwa uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu baada ya kusikilizia hoja za pande zote, katika uamuzi wake ilioutoa Juni 28, 2021, imekubaliana na hoja za wadaiwa na kuridhia uamuzi wa mamlaka za Serikali za kumtengua katika kiti hicho.

Hivyo mahakama hiyo iliondoa amri yake ya zuio la muda ililotoa Aprili 28, mwaka huu na kuruhusu mchakato wa uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo uendelee.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Athuman Matuma amesema kwamba baada ya kusikiliza pande zote ameridhika kuwa diwani huyo alitenguliwa katika nafasi hiyo kutokana na ripoti ya uchunguzi wa idara ya Uhamiaji kuhusiana na uraia wake na kwamba naye alikuwa na taarifa za uchunguzi huo ndio maana hakupinga kuhojiwa kwa suala hilo.

Jaji Matuma alisema kuwa Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya Ndani ndio wanahusika na uraia wa mtu.

Alibainisha kuwa kwa kuwa mamlaka hizo hazikuwa miongoni mwa wadaawa katika shauri hilo, basi uamuzi wake kuhusiana na hadhi ya uraia wake haiwezi kuvurugwa wala kuhojiwa kwa sababu ya msingi wa kanuni tu kwamba hakuna mtu anaweza kuhukumiwa bila kusikilizwa kama uamuzi wake ulikuwa sahihi au la mbele ya sheria.

“Kwa hiyo wakati mwombaji alipojulishwa na mdaiwa wa nne (Mkurugenzi) kwamba kiti chake cha udiwani kilikuwa wazi kwa sababu za uraia wake, alipaswa kufuatilia uamuzi wa uraia wake huo na kuupinga kabla ya kupigania udiwani wake kwa kuwa uraia ndio sifa ya msingi katika nafasi za kisiasa kama udiwani,” alisema Jaji Matuma.

Amesema kuwa mwombaji ana haki ya kuhoji uamuzi wa uraia wake kwa mujibu wa sheria.

“Kwa msingi huo, amri yangu ya Aprili 28, 2021 kuwazuia wadaiwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi mdogo imefikia mwisho leo na wanaweza kuendelea,” alihitimisha Jaji Matuma.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post