Serikali ya Tanzania imesema ulifanyika utafiti wa kutosha kabla ya kuanzisha tozo za miamala ya fedha za simu na kadi za simu zinazolalamikiwa kwa sasa nchini humo.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja muda mfupi baada ya Kiongozi wa chama cha Upinzani cha CHADEMA, Freeman Mbowe, na baadhi ya wasomi na wananchi wanaokosoa tozo ama kodi hizo kusema hakukufanyika utafiti wa kutosha kuzianzisha. Tozo ya miamala inalalamikiwa kutokana na kudaiwa kuwa na makato makubwa huku tozo ya kadi za simu ikitarajiwa kuanza kufanya kazi Agosti Mosi mwaka huu.
Waziri wa fedha Tanzania, Mwigulu Nchemba ameiambia BBC kwamba pamoja na kusema tozo hizo zitaangaliwa ila amefafanua kwamba uwepo wake ni sheria ya Bunge, ambayo yeye kama Waziri hawezi kuzifuta ama kuziondoa, kitakachofanyika kwa sasa ni kupitiwa kwa kanuni kuangalia kama utekelezaji wake unafanyikakwa njia isio ya kirafiki. Amezungumza na mwandishi wetu Martha Saranga.