Luiza Nyoni Mbutu ni mama na mke - anajulikana sana pia kama Mwanamuziki na mwanadensi nchini Tanzania , akiwa ni mmojawapo wa wanawake waliodumu sana kwenye fani hii kwa miaka mingi .
Luiza anaadhimisha miaka 22 ya kuwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta alioanzisha Dar es Salaam Tanzania .
Katika kipindi hicho kirefu ambacho amekuwa muimbaji na pia mcheza densi wa bendi hii anasimulia pandashuka katika tasnia ya burudani fani ambayo ameitumia kujikimu kimaisha na huifanya wakaio wa usiku .Ari na hamu yake kuwaburudisha watu ndio msukumo mkubwa aliyo nao kuifanya kazi yake .
Ila haijakuwa barabara iliyonyooka hasa akiwa ni mwanamuziki wa densi ambaye ni wa kike katika jamii ambayo bado inaanza kupokea wanawake walioko katika fani hii kwa shauku .
"Nilitaka niwe mwanamuziki , kwa kuwa nilipenda muziki ila tangu mwanzo nilitaka niwe mwanamuziki mwenye mfano uliyo tofauti na jinsi wanawake wengine waliokuwa kwenye bendi nyakati hizo walivyokuwa , jamii iliwachukulia kama wahuni na wasiokuwa na nidhamu "anasema Luiza
Safari yake ilianzaje?
Luiza alizaliwa Dar es Salaam laini asili yake ni Kusini mwa Tanzania katik mkoa wa Lindi ambako wazazi wake wanaishi . Wamezaliwa watoto sita na
dada yake mkubwa ndiye aliyemtangulia katika muziki wa bendi .Luiza tangia utotoni alikuwa anacheza ngoma , aliingia kwenye vikundi vya utamaduni na burudani akiwa shule ya msingi .
Na hata wakati huo alikuwa anamuomba Mungu aweze kufika ngazi ya juu ya muziki. Akiwa mtoto hakuwa anaogopa kusimama mbele ya watu kutoa burudani na hivyo ndivyo ilivyogundulika .
Bendi ya African stars Twanga pepeta imesifika sana kutokana mtindo wa densi zake kwa miongo miwili sasa na bendi hiyo inayoongozwa na Luiza inajizatiti kuwa kwenye ushindani na miziki ya kisasa .
Mtihani wa kuimba kanisani na Kwenye Vilabu
Kabla ya Luiza hajaanza kuimba kwenye bendi , alikuwa ni mshiriki wa Kwaya katika kanisa alilokuwa anashiriki. Hakudhania kuwa uamuzi wake wa kuwa mwanachama wa bendi ya Twanga Pepeta ingezua mtafaruku mkuu ndani ya kanisa lake .
"Wakati huo nilikuwa chipukizi, nilikuwa naimba kwaya kanisani , wale viongozi wetu pale kwenye kwaya walipofahamishwa kuwa nilikuwa ninaimba kile kinachotajwa kuwa nyimbo za kidunia , ilikuwa ni shida kubwa . Washirika waliuliza kwanini kwenye kwaya yetu tuna mtu anaimba nyimbo za dunia hatumtaki kabisa."Anakumbuka Luiza
Kesi ile iliendelea na kuwa kubwa hadi kusababisha mpasuko mkubwa katika kwaya alioishiriki Luiza . Upande mmoja kuna wale waliokuwa wanamuunga mkono mwanadada huyu , na upande wa pili kuna wale waliohoji kuwa hawezi kuimba nyimbo za dini na bado aimbe kwenye majukwaa ya nyimbo za dunia .Ni msimamo uliyochukuliwa hata na wasimamizi wa kanisa lile .
"Watu waliokuwa na shida na mimi kuendelea kuimba kwenye kwaya kanisani walikuwa na maoni kwamba , nimekuwa mwanamuziki wa nyimbo za dunia , nitaanza kuvalia nguo zisizokuwa na heshima , nitakuwa mlevi , na nitaanza kuwa na tabia mbaya'.
Anaongeza 'Hata hivyo hakuna chochote kilichobadilika kunihusu . Nikiwa kwenye kwaya nilivalia sare za kwaya , nikiwa kwenye bendi nilikuwa navalia sare za bendi na baada ya kumaliza muziki nazivua papo hapo"anakumbuka Luiza .
Bi. Luiza anasema kuwa aliyasikia memngi ya watu kuhusu hatua yake ya kuimba katika bendi na jinsi wenzake katika kwaya walivyomgeuka .
Alianza kuimba katika kwaya akiwa darasa la tatu hadi wakati alipokuwa mtu mzima . naongeza kuwa wakati mambo yalipozidi kanisani aliamua alijiondoa kutoka kwaya ya kanisa .
Dhana kuhusu wanamuziki wa kike sio nzuri
Luiza anasema , kuwa mwanamuziki wa na mwanadensi ambaye amebobea nchini Tanzania kwa miaka anayoanza kazi ile , ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwani jamii , ilikuwa na maoni tofauti kuhusu wanamuziki wa kike wenye kuingia ulingo wa densi na sanaa ya muziki .
Ila Luiza anasema kuwa dhana hizo zilikuwepo kutokana na sababu za wanawake waimbaji wachache ambao walipotoka kimaadili wala sio wote .
"Nikianza ilikuwa ni kiza kikuu kwani jamii haikunielewa , wala hata pale kanisani wengi waliuliza ni kwanini nimeamua kuingia kwenye fani ya densi na muziki ilhali nilikuwa na vyeti? Rafiki yangu mmoja alinisogelea na kuniuliuza kwanini nisitafute kazi nyengine badala ya kuimba lakini mimi sikukata tamaa niliendelea kuamini kuwa ndoto yangu ilikuwa halisi "anakumbuka Luiza
Mwanadada huyu anasema mashabiki wa nyakati hizo pia hawakuwapokelea vyema waimbaji wa kike katika bendi . Kwa mfano anasema jinsi mashabiki walivyokuwa wakitoa pesa zao kuwazawadi wanamuziki ,ilikuwa kupitia njia inayoonekana kuwavunjia heshima.
"Kwa mfano wakati shabiki anataka kutoa hela kwa jili ya kufurahia wimbo au densi wakati anampa mwanamume muimbaji atampa kwa heshima kupitia mikono yake , ila ikiwa kwa mfano ni mimi atakuwa anang'ang'ana kunikia kifuani kuziingiza katika matiti yangu ..hizo ni baadhi ya tabia tulizozipigana hadi zikafika kikomo "anasema Luiza
Mwanamke huyu anasema kuwa leo hii huwezi kumuona shabiki akifanya tabia hizo , kwani siku hizi wale wanaofanya hivyo huonekana kama "mashabiki washamba" ambao hawajazoea burudani katika vilabu.
Anaongeza kuwa muziki umemfikisha mbali kwa miaka zaidi ya ishirini ambayo amejitosa kwenye fani hiyo , ndio kitu ambacho amekitumia kukithi mahitaji yake ya kila siku kando na kuubeba muziki taaluma yake kubwa .
Luiza anasema kuwa amefaidika kwa kutumbuiza watu nje na ndani ya Tanzania na safari zake nje ya nchi zimemfanya kukomaa mawazo kwani anatangamana na wanamuziki w kimataifa na kusoma mengi .
Maisha ya Ndoa
Luiza anasema kuwa huenda alibahatika mno , kwani alikutana na barafu ya moyo wake , ambaye sasa ni mume wake na baba ya mtoto wake , katika mazingira hayo ya kazi ya uimbaji na unenguaji .Ikiwa sasa ni miaka 22 tangu wawili hao waanze maisha ya ndoa Luiza anasema kuwa inawezekana hata wanawake wasanii wakawa kwenye ndoa zao hadi mwisho .
"Wakati mwingi wanawake hasa wasanii wanapoingia kwenye maisha ya ndoa , hujipata wamesahau talanta na vipaji vyao , na badala yake wanaanza kutekeleza majukumu ya kifamilia na wakati mwingi kujisahau'
Anaongeza : 'Tangu mwanzo nilimuonyesha mume wangu kwamba talanta yangu ya uimbaji ni muhimu na licha ya kuingia kwenye ndoa bado nitaendelea kuwa mwanamuziki" anatamatisha Luiza