Mawakili wa serikali nchini Morocco wamesema nchi hiyo imewasilisha kesi ya kuchafuliwa jina dhidi ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International na shirika moja lisilo la kiserikali la Ufaransa. Mawakili hao wanasema mashirika hayo yanadai kwamba shirika la ujasusi la Morocco lilitumia programu ya udukuzi ya Pegasus dhidi ya waandishi kadhaa wa habari wa Ufaransa. Mawakili wa serikali ya Ufaransa nao walianzisha uchunguzi wao wenyewe wiki hii kufuatia madai ya Amnesty International na Shirika la habari la Forbidden Stories yaliyochapishwa na mashirika kadhaa ya habari yakiwemo gazeti la Washington Post na gazeti la kila siku la Ufaransa, Le Monde. Kesi hiyo itatajwa kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 8 mjini Paris ingawa haitosikilizwa hadi baada ya miaka miwili.