Msichana auawa kwa kuvaa jeans India

 

Jeans

CHANZO CHA PICHA,RAJESH ARYA

Taarifa za wasichana na wanawake wenye umri mdogo kushambuliwa kikatili na wanafamilia hivi karibuni zimekuwa zikigonga vichwa vya habari nchini India.

Matukio hayo pia yameangazia jinsi wasichana na wanawake wanakosa usalama hadi ndani ya nyumba wanazoishi na familia zao.

Wiki iliyopita, Neha Paswan, mwenye umri wa miaka 17, anadaiwa kupigwa hadi kufa na watu wa familia yake katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh kwasababu hawakupenda vile anavyovaa jeans.

Mama yake, Shakuntala Devi Paswan, aliiambia BBC Hindi kwamba msichana wake alikuwa amepigwa vibaya na fimbo na babu yake na wajomba zake baada ya kutokea kwa mabishano nyumbani juu ya nguo zake anazovaa katika kijiji cha Savreji Kharg wilayani Deoria, moja ya maeneo yenye maendeleo duni katika jimbo hilo.

"Alikuwa amefunga siku nzima kwendana na dini. Wakati wa jioni, akavaa suruali ya jeans na juu akawa na top au aina ya fulana kufanya ibada zake. Wakati babu na bibi yake walipinga mavazi yake, Neha alijibu kwamba jeans zilitengenezwa kwa ajili ya watu kuvaa", mama yake alisema.

Hoja hiyo ilizidi na kusababisha vurugu, anadai.

Shakuntala Devi alisema wakati binti yake akiwa amelala baada ya kupoteza fahamu, wakwe zake waliita gari wakisema wanampeleka hospitalini.

"Hawakuniruhusu niandamane nao kwa hivyo niliwatahadharisha jamaa zangu ambao walikwenda hospitali ya wilaya wakimtafuta lakini hawakumpata"

RAJESH ARYA

CHANZO CHA PICHA,RAJESH ARYA

Asubuhi iliyofuata, Shakuntala Devi alisema, walisikia kwamba mwili wa msichana mmoja umepatikana ukininginia kutoka kwenye daraja juu ya mto wa Gandak unaopita eneo hilo.

Walipokwenda kuchunguza, waligundua mwili huo ni wa Neha.

Polisi wamewasilisha kesi ya mauaji na uharibifu wa ushahidi dhidi ya watu 10, akiwemo babu na nyanya wa Neha, ami, shangazi, binamu na dereva wa magari.

Washtakiwa bado hawajatoa tamko lolote kwa umma.

Afisa mwandamizi wa polisi Shriyash Tripathi aliambia BBC Hindi kwamba watu wanne, pamoja na babu na nyanya, mjomba na dereva wa magari, wamekamatwa na walikuwa wanahojiwa.

Alisema polisi walikuwa wakiwatafuta washtakiwa waliosalia.

Babake Neha, Amarnath Paswan, ambaye hufanya kazi kama mfanyakazi wa siku katika maeneo ya ujenzi huko Ludhiana, mji wa Punjab, alikuwa amerudi nyumbani kukabiliana na msiba huo na kusema alijitahidi kupeleka watoto wake shuleni ikiwa ni pamoja na Neha.

Shakuntala Devi alisema binti yao alitaka kuwa afisa wa polisi, lakini "ndoto zake sasa zimekatizwa".

Alidai kwamba wakwe zake walikuwa wakimshinikiza Neha aache masomo yake katika shule ya eneo hilo na mara nyingi alimshtaki kwa kuvaa nguo nyingine tofauti na mavazi ya kitamaduni ya Kihindi.

Neha alipenda kuvaa mavazi ya kisasa - picha mbili ambazo familia yake ilishirikisha BBC ilimwonyesha amevaa gauni refu katika moja na suruali ya jeans na koti katika picha nyingine.

Wanaharakati wanasema unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana ndani ya nyumba kwenye jamii iliyozama katika mfumo dume, mara nyingi maamuzi huidhinishwa na wazee wa familia.

Wasichana na wanawake nchini India wanakabiliwa na vitisho vikali - kutokana na kuwa katika hatari ya kuuawa hata kabla hawajazaliwa kwasababu ya upendeleo wa wana wa kiume - kwa ubaguzi na kupuuzwa.

Vurugu za nyumbani zimeenea na kwa wastani, wanawake 20 wanauawa kila siku kwa kuleta mahari ambayo haijatosha.

Wanawake na wasichana katika mji mdogo na vijijini nchini India, wanaishi chini ya vizuizi vikali na wakuu wa vijiji au wazee wa familia mara nyingi wanaamuru ni nini wanafaa kuvaa, wanaenda wapi au wanazungumza na nani, na hatua yoyote mbaya inayodhaniwa kuwa kinyume, inachukuliwa kama uchochezi na lazima aadhibiwe.

Haishangazi basi kwamba shambulio linalodaiwa kutekelezwa dhidi ya Neha kwa chaguo lake la mavazi ni moja tu kati ya mashambulio ya kikatili yaliyoripotiwa juu ya wasichana na wanawake wadogo na wanafamilia ambayo yameshtua India.

Mwezi uliopita, video iliyoumiza wengi ambayo ilitokea wilaya ya Alirajpur katika jimbo jirani la Madhya Pradesh, ilionyesha mwanamke wa kabila fulani mwenye umri wa miaka 20, akipigwa na baba yake na binamu zake watatu wa kiume.

Kufuatia hasira iliyojitokeza kwa umma, polisi waliwasilisha malalamiko dhidi ya wanaume hao waliosema msichana huyo alikuwa "akiadhibiwa" kwa kutoroka ndoa yake alikokuwa anapitia"unyanyasaji".

Wiki moja kabla ya tukio hilo, ripoti zilisema wasichana wawili walipigwa bila huruma na wanafamilia wao kwa kuzungumza kwa simu na binamu wa kiume katika wilaya jirani ya Dhar.

Video za tukio hilo zilionyesha mmoja wa wasichana akiburutwa kwa kushikwa nywele zake, akatupwa chini, akapigwa teke na ngumi na kupigwa kwa fimbo na mbao mbao na wazazi wake, kaka na binamu.

Baada ya video hiyo kuenea, polisi waliwakamata watu saba.

india

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Tukio kama hilo - ambalo pia lilifanyika mwezi uliopita - limeripotiwa kutoka jimbo la Gujarat ambapo vijana wawili walipigwa na watu wasiopungua 15, wakiwemo jamaa zao, kwa kuzungumza kwenye simu za rununu, polisi walisema.

Mwanaharakati wa jinsia Rolly Shivhare anasema "inashangaza kwamba katika karne ya 21, tunaua na kushambulia wasichana kwa kuvaa vazi la jeans au kuzungumza kwa simu za mkononi."

Mfumo dume, anasema, ni "moja wapo ya shida kubwa nchini India", na anasema kuwa wanasiasa, viongozi na washawishi mara nyingi hutoa maoni potofu ambayo yanaonyesha mfano mbaya na kupitisha ujumbe kwamba usawa wa kijinsia hauchukuliwi kwa uzito mkubwa na jamii na familia.

"Serikali inasema wasichana ndio kipaumbele chetu na inatangaza miradi mikubwa kwa ustawi wao, lakini hakuna kinachotokea katika uhalisia wa maisha," Bi Shivhare anasema.

Magharibi, mtoto au mwanamke aliye katika hatari ndani ya nyumba zao anaweza kuhamishiwa kwenye makao au kuwekwa katika nyumba za kutunza watoto.

"Nyumba za makazi na vituo vya kuwatunza nchini India ni vichache na vingi vinaendeshwa vibaya hivi kwamba hakuna mtu atakayetaka kuishi huko. Serikali yetu inahitaji kutenga fedha zaidi na kuboresha hali zao", Bi Shivhare anasema.

"Lakini suluhisho pekee la muda mrefu ni kuwafanya wasichana wafahamu zaidi haki zao."

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post