Tanzania kupewa chanjo ya corona chini ya mpango wa Uholanzi

 


Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika zitakazonufaika na mpango wa chanjo unaosimamiwa na Serikali ya Uholanzi.

Uholanzi imetenga dozi 750,000 za chanjo aina ya Astrazeneca kwa ajili ya nchi zenye mahitaji ikiwemo Tanzania na Namibia. Dozi hizo zimehifadhiwa tayari kwa ajili ya kusambazwa kwa nchi hizo zilizoonyesha nia ya kusaidiwa.

Uholanzi kupitia mamlaka zake za afya inachangia chanjo kusaidia nchi masikini kukabiliana na virusi vya Corona, ikifanya hivyo pia kwa kuchangia karibu dozi nusu milioni kwenye mpango wa chanjo kwa nchi masikini (Covax).

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu Uholanzi inatarajiwa kuchangia dozi milioni 20 kwenye mpango huo.

Mbali na Tanzania, Cape Verde na Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na hatua hiyo ya Uholanzi.

Mapema mwezi huu, Uholanzi ilitangaza kuipa Indonesia dozi milioni 3 za chanjo hiyo, ingawa haijafahamika wazi, ni kiwango gani cha chanjo zitapelekwa Tanzania na Namibia,

Serikali ya nchi hiyo imeeleza kuwa wizara yake ya afya itasimamia usambazaji wake kuzifikia nchi hizo.

Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi chache duniani ambazo hazikuwa zimekubali chanjo ya Corona, hasa kutokana na msimamo wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, aliyekuwa anazitilia shaka chanjo za corona, akitaka ufanyike utafiti wa kina kabla ya kuzikubali.

Wakati upande wa pili wa Muungano, Zanzibar ukiendelea kutoa chanjo, Serikali ya Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan iko katika hatua mbalimbali za kuingiza chanjo mbali mbali za corona ambazo zitatolewa kwa uhuru kwa wananchi wake.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post