Polisi jijini Dar es Salam wamewatawanya wafuasi wa Chadema ambao walikuwa wamekusanyika nje ya mahakama ya Kisutu kufuatilia kesi ya mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa nia ya mtandao hata hivyo imeahirishwa kutokana na changamoto za kimawasiliano. Mbowe anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho asubuhi kuendelea na kesi hiyo.
Awali wafuasi wa Chadema walionekana nje ya mahakama hiyo wakiwa na mabango yaynaosema: 'Mbowe sio gaidi’ na pia walikuwa wakipaaza sauti na kusema, ‘katiba mya sio ugaidi’.
Hata hivyo polisi waliwatawanya wafuasi hao na baadhi yao kukamatwa.
Mawakili wa Mbowe wakiongozwa na Peter Kibatala , wapo mahakamani hapo lakini mteja wao ni mahabusi katika gereza la Ukonga.
Mbowe anakabiliwa na mashtaka ya kuhujumu uchumi na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Wakosoaji wa serikali ikiwemo Chadema pamoja na mashirika ya haki za kibinadamu wanaichukulia kesi hiyo ni ya kisiasa na kushinikiza serikali imwachie huru mwanasiasa huyo.
Hata hivyo polisi wamekanusha madai hayo na kwamba wanasema wana ushahidi wa kutosha kwamba Mbowe alitenda makosa hayo na kutaka mahakama iachwe itekeleze wajibu wake.