Rodrigo Duterte alichaguliwa kuwa rais wa Philippines mnamo mwaka 2016 kwa ushindi wa kishindo akiahidi kupambana na masuala ya uhalifu pamoja na rushwa.
Tangu wakati huo ameingia kwenye mijadala ya masuala tata kuhuu vita iliyojaa damu dhidi ya dawa za kulevya na matamsha yake yanayotazamwa na wengi kama yana utata na yanayodhalilisha
Amekuwa pia akiandamwa na kukosolewa na jamii za kimataifa kwa wanaharakati wa haki za binadamu wanaoona sera zake nyingi zinakuka haki za binadamu,
Pamoja na kwamba amekuwa akikosolewa na vitendo vyake kulaaniwa na jumuia mpaka za kimataifa, amendelea kuwa mtu mwenye umaarufu mkubwa nchini kwake Philippines.
Kuwachinja wanaotumia dawa za kulevya
Miaka ya mwanzo kabisa ya utawala wa Duterte kama rais, ilijaa sifa ya ukandamizaji usiokoma kwa watu wanaodaiwa kuuuza ama kutumia dawa za kulevya
Akiwataka wananchi na Polisi kuongeza jitihada zaidi za kuwashughulikia ikiwemo hata kuwaua washukiwa wa makosa hayo na maelfu wameuawa kwa watu kujichukulia sheria mkononi katika kampeni hiyo ya kupambana na dawa za kulevya.
Kukiwa na watumiaji wa dawa za kulevya zaidi ya milioni 3 nchini Philippines, Rais Duterte anasema atakuwa na 'furaha ya kuwachinja'.
Rais huyo anasema msimamo wake huo mkali ni muhimu katika kumaliza kabisa bishaara haramu ya dawa za kulevya na kwamba anaona inawezekana na hajakata tamaa, akiapa 'kuua' kila anayejihusisha na biashara hiyo.
Katika kipindi kifupi tangu azindue mpango wake wa kukabiliana na dawa za kulevya baada ya kuingia madarakani iliripotiwa kwamba karibu watu 6,000 waliuawa na Polisi, watu wanaojichukulia sheria mkononi na askari waliokodishwa kutoka nje ya nchi.
Umoja wa mataifa, Kanisa la Katoliki, Umoja wa Ulaya na Marekani mara kadhaa wamelazimika kulaani sera za kiongozi huyo zinazokiuka misingi ya haki za binadamu. Wanaharakati wa ndani pia wamekuwa wakikosoa na kupinga mauaji hayo yanayoendelea nchini humo.
Aliwahi kukiri kuua watu kwa mikono yake
Katika moja ya mahojiano yaliyoibua hisia kati yake na BBC, mwishoni mwa mwaka 2016, Rais Duterte aliwahi kuthibitisha kuwapiga risasi na kuua watu watatu wakati akiwa meya wa jiji la Davao.
Alisema: "Niliua watu kama watatu... sijui risasi ngapi zilitoka kwenye bunduki yangu na kuingia katika miili yao. Ilitokea na siwezi kudanganya kuhusu jambo hili."
Utata ulianza mapema alipowaambia wafanyabashara waliofika Ikulu kwamba
"Nikiwa Davao nilikuwa naua mwenyewe. Kuwaonyesha tu Polisi kwamba kama mie naweza kufanya vile kwanini wao washindwe.
"Nilikuwa nazungumza Davao kwa bodaboda, kwa baiskeli kuangalia hali ya mambo mitaani, kuangalia kama kuna shida. Nilikuwa naangalia kama kuna shida imejitokeza ili niue."
Kauli tata za Duterte na utani wake wa kuudhi
Licha ya watu kuzidi kumkosoa, Duterte anayejulikana kwa kutoa matamshi tata, amekuwa akijibu mapigo na kuonyesha kuendelea na mapambano yake.
Amewahi kutishia kujiondoa Umoja wa Mataifa, ambapoa baada alisema kwamba alikuwa akitania na kumwita Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon "ni mjinga".
Aliwahi kuwaita pia Umoja wa Ulaya (EU) kwamba ni "wanafiki" wakati akitoa hotuba yake na kuonyesha pia kidole cha kati, kinachoelezwa kwamba ni matusi.
Aliwahi kumuita rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kama "mtoto wa kahaba", lakini baadae alionyesha kusikitika wakati Obama alipositisha kukutana naye.
katika nchi ambayo Kanisa Katoliki limekuwa likijitolea sana kusaidia, bila wasiwasi Rais huyo aliwahi kumuita papa "ni mtoto wa kahaba" na kusema Mungu alikuwa 'mjinga'.
Rais Duterte alileta utani kwamba wakati alikuwa bado ni meya wa kusini mwa jiji la Davao angepaswa kuwa wa kwanza kumbaka Mmishonari wa Austraria aliyeuawa kwenye moja ya ghasia gerezani.
Kumekuwa na okosoaji mkubwa kufuatia matamshi yake kwamba aliwahi kumnyanyasa kingono mtumishi wa kazi wakati akiwa kijana na kumbusu hadharani kwenye jukwaa mfanyakazi wa kike, ikielezwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Gabriela kama Rais anayenyanyasa wanawake na kufanya mambo ya kuchukiza na kuudhi dhidi yao.
Corona inazidi kuonyesha sura halisi ya Duterte
Ikiwa na visa vya wagonjwa wa corona wapatao milioni 1.3, Phillipines inapambana na hali mbaya ya maambukizi ya Covid 19 yanayosumbua sana Asia na dunia kwa ujumla. Rais huyo amekuwa akitoa kali kali kuhusu watu wasioataka kuchanjwa na wiki jana alisema raia wa nchi hiyo wasiotaka kuchanjwa dhidi ya Corona kusalia majumbani mwao .
Alisema nchi yake imechukua hatua ya kuwachanja wanaotaka kupokea chanjo hiyo huku akiongeza kwamba wasiotaka kuchanjwa wakifa basi yeye hajali .
' Kwa wale watu ambao hamtaki kuchanjwa nawaambia msitoke nyumbani kwenu.Ukitoka nyumbani kwako ,nitawaambia polisi wakurejeshe ndani.Utasindikizwa kurejea kwako kwa sababu wewe ni msambazaji anayetembea wa virusi hivi …Iwapo hutaki kuchanjwa basi usitoke kwako..tuwape chanjo wanaozitaka… na wasiotaka kuchanjwa basi mnaweza kufa wakati wowote,mimi sijali'
Mpaka mwezi June, watu million 2.1 tu nchini humo walikuwa wamechanjwa kati ya watu milioni 70 waliolengwa kuchanjwa mwaka huu.
Kwa Rais Duterte hilo ni tatizo na akaeleza wazi kwa watu wanaokataa kuchanjwa atawatia ndani.
"Chagua upate chanjo,ama nitakufunga jela," Duterte alisema kwenye moja ya hotuba zake za mwezi uliopita kutokana muitikio mdogo wa watu kwenda kupata chanjo hasa kwenye jiji la Manila.
Licha ya kukosolewa namna anavyolazimisha watu kupata chanjo Rais huyo akatishia kuwachoma matakoni sindano zenye dawa ya kutibu nguruwe badala ya binadamu.
"Kama uko hapa na binadamu unayeweza kupata virusi, nenda kapate chanjo, vinginevyo nitaamuru viongozi wote wa vijiji kuwaorodhesha wote wanaokataa kuchanjwa. Kwa sababu kama si hivyo, nitaruhusu mchomwe sindano za nguruwe."
Mbali na hilo, kiongozi huyo mtata aliwataka wote wanaokataa kuchomwa chanjo ya corona, waondoke nchini humo kwenda India ama nchi yoyote ya Amerika.
Chimbuko lake kwenye siasa
Rodrigo "Digong" Duterte alizaliwa mwaka 1945 katika familia iliyokuwa karibu na siasa. Baba yake aliwahi kuwa gavana na familia hiyo ilikuwa na uhusiano mkubwa na familia zenye ushawishi katika jimbo la Cebu province, wakati baba yake alipokuwa meya.
Duterte alisomea sheria na alianza kama mwendesha mashitaka wa serikali, kabla ya kuwa Meya wa Davao mwaka 1988, akatawala jiji hilo kwa miaka zaidi ya 30
Akakijengea heshima kwa kushughulikia matatizo makubwa yaliyokuwa yanawasibu rais wa Philippines kama uhalifu, matumizi ya mabavu na rushwa. Masuala haya matatu yakawa kipindi hicho yalifanya jiji hilo la Davao, kuwa moa ya majiji salama nchini Philippines.
Rekodi yake hiyo ya Davao ikamsaidia kupata ufuasi nchi nzima, ambapo watu wengi walikua na imani kwamba anaweza kushughulikia masuala hayo pia kwa ngazi ya kitaifa.
Duterte kusalia madarakani kwa mlango wa nyuma?
Mwakani ni ukomo wa kipindi cha miaka 6, cha utawala wa Duterte, lakini haitashangaza kuona akiwa rais tena baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
Kwa mujibu wa Reuters Duterte alishawahi kuonyesha ishara kwamba anaunga mkono wazo la kuwania nafasi ya Makamu wa Rais.
Lakini kwa mwanasheria Christian Monsod, mmoja wa watu waliohusika kwenye mchakato wa kubadili katiba ya 1987, anasema kwamba dhamira ya Duterte ya kurejea madarakani iko wazi.
"Kuna mpango atumie mlango wa nyuma kubaki madarakani," Alisema Mwanasheria huyo Monsod, aliyekuwa mkuu wa tume ya uchaguzi na kumtaka aheshimu katibu.
Si Msemaji wa Duterte, wanasheria wake au Duterte mwenyewe amezungumzia kuhusu hilo.
Duterte, anayeonyesha kana kwamba haitaji kuendelea kukaa madarakani, anataka 'swahiba' wake na msaidizi wake wa muda mrefu wa masuala ya habari, Christopher "Bong" Go amrithi.
Kumuunga mkono Go kulisaidia akashinda useneta mwaka 2019 kazi ambayo aanaifanya huku akiendelea kuwa mmsaidizi wa karibu wa Duterte. Hata hivyo Go anasema hana mpango wa kugombea.
Binti wa Duterte, ambaye ni meya wa Davao Sara Duterte-Carpio alimpiku Go kwenye kura za maoni za mtu anayeweza kuwa rais ajaye wa nchi hiyo. Pamoja na hilo, Sara mwenyewe na baba yake Duterte hwaungi mkono wazo la binti huyo kugombea urais.
Mabadiliko ya katiba
Akijiweka kwenye kundi la wajamaa na mpenda mabadiliko, akahaidi kuibadilisha nchi hiyo kutoka kwenye mfumo wa kila kitu kuamua na serikali kuu na kuwa nchi ya Kibunge, kwa kulipa nguvu bunge, ili kuwa na mgawanyo bora wa utajiri na mapato ya nchi hiyo.
Kuungwa mkono na wafuasi wake kisiasa katika ushindi wa kishindo wa uchaguzi wa maseneta wa mwaka 2019 ukamfanya kuongoza bunge la seneti ambalo ni la juu kwa maamuzi
Hilo linamaanisha kwamba anaweza kupitisha mipango yake ya kubadili katiba na kuifanya nchi hiyo kufuata misingi ya shirikisho
Hata hivyo wakosoaji wanasema bila kubadilisha mifumo katika ngazi za chini za vijiji na mikoa, mabadiliko anayoyataka kwa ngazi ya kitaifa itaweza kuwapa mamlaka yasiyodhibitiwa kikundi cha watu wachache.
Uwingi wa wabunge wa seneti wanaomuunga mkono kunamruhusu kupitisha na sera zake zenye utata kama kurejesha adhabu ya kifo au kupunguza umri wa mtu anayeweza kuwajibika dhidi ya makosa ya kihalifu.