Taarifa za hivi punde ni kwamba Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amevaa Gwanda za Jeshi na kuingia "Uwanja wa Vita" kutetea nchi yake
Majeshi ya Urusi yameripotiwa kuzidi kuingia katika Mji Mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Awali, kulikuwa na tetesi kuwa Rais huyo amekimbia nchi, ambapo alijitokeza na kuomba Wananchi wapuuzie taarifa hizo akisema kufa na kupona watapambana na Urusi mpaka hatua mwisho.
Aidha Rais Volodymyr Zelensky amekataa ofa ya Marekani ya kumsaidia kuondoka Ukraine ili kuokoa maisha yake wakati majeshi ya Urusi yakiwa yameuzingira mji huo ambapo amenukuliwa akisema;
"Unapotushambulia, utaona nyuso zetu, siyo migongo yetu".
Shirika la Habari la Associated Press limeeleza likimnukuu afisa mmoja wa kijasusi kutoka Ikulu ya White House ya Marekani, akieleza kwamba rais huyo amekataa ofa ya kutoroshwa na Marekani na kuahidi kuendelea kuipigania nchi yake mpaka tone lake la mwisho la damu.
Msimamo wa Volodymyr wa kuamua kuingia mwenyewe mstari wa mbele wa vita, umesifiwa na wengi hususan katika mitandao ya kijamii, hasa baada ya kujirekodi kipande cha video na kukanusha habari zilizokuwa zinaenezwa mitandaoni kwamba ameikimbia nchi yake.
